Klabu ya soka ya Uingereza, Chelsea, imeshinda Kombe la Dunia la Vilabu kwa kuichakaza klabu ya soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain bao 3-0 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa usiku wa kuamkia leo nchini Marekani.

Ushindi huo wa Chelsea kwenye dimba la MetLife mjini New Jersey umewaacha wengi vinywa wazi. Licha ya kutinga fainali kulikuwa na matumaini madogo miongoni mwa wachambuzi wa soka duniani kuwa Chelsea ingemudu kulitwaa kombe hilo mbele ya PSG, ambayo mwezi Mei walinyakua kombe la michuano ya klabu bingwa barani Ulaya, Champions League.

Hata hivyo magoli mawili ya Cole Palmer na jingine la Joao Pedro yaliyotiwa wavuni mnamo dakika 45 za kwanza yalisadifu kuwa kihunzi ambacho PSG walishindwa kukivuka.

Kufuatia ushindi huo Chelsea imeweka kibindoni kitita cha dola milioni 120 kinacholewa na Shirikisho la Kandanda Duniani, FIFA.