China imefanya gwaride kubwa la kijeshi katika uwanja wa Tiananmen jijini Beijing kuadhimisha miaka 80 tangu kushindwa kwa Japan mwishoni mwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Gwaride hilo limetasfiriwa na wachambuzi kama ishara ya mabadiliko ya nguvu za kisiasa, kiuchumi na kijeshi duniani ambapo China – chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping – inajitokeza kama taifa lenye uwezo wa kuongoza utaratibu wa dunia, nafasi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikishikiliwa na Marekani.

Gwaride hilo linafanyika katika uwanja wa Tiananmen kuadhimisha miaka 80 tangu kushindwa kwa Japan mwishoni mwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Rais Xi Jinping ameongoza hafla hiyo akiwa amezungukwa na Rais wa Urusi Vladimir Putin na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.

Hafla hiyo iliyopewa jina la “Siku ya Ushindi” inafanyika katika wakati ambapo China na Marekani zinakabiliwa na mvutano wa kibiashara.

Alipoulizwa kuhusu tafsiri ya gwaride hilo, Rais wa Marekani Donald Trump amesisitiza kuwa ana uhusiano mzuri na Rais Xi Jinping, akiongeza kuwa China inaihitaji zaidi Marekani kuliko jinsi Marekani inavyoihitaji China.

Hata hivyo, viongozi wa Magharibi hawakuhudhuria hafla hiyo, hatua inayoonesha msimamo wao kuhusu sera za China hususan katika masuala yanayohusu haki za binadamu, kisiwa cha Taiwan na mvutano wa kijeshi katika Bahari ya Kusini ya China.