Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Rufiji
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Rufiji, ambae pia ni Diwani wa Kata ya Shela Abdul Chobo, amewataka watumishi wa umma kushirikiana katika kutatua changamoto zilizopo kulingana na taaluma zao, ili kuiinua jamii katika sekta mbalimbali.
Akizungumza wakati wa kikao chake cha kwanza na watumishi hao kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mohoro, Disemba 10, 2025, Chobo alisema hatua ya kuanza kukutana na watumishi inalenga kuweka misingi ya ushirikiano wa kazi na kupanga mikakati madhubuti ya maendeleo ya kata.

“Ninatambua umuhimu wenu, nimewaita kuwaomba ushirikiano katika kazi hii niliyopewa”
” Kila kada iniambie nini tufanye ili tufanikiwe, kama ni elimu, tuainishe changamoto zilipo ni eneo gani mimi nisimame kama kiongozi, na ninyi kama wataalamu msimamie wapi, tuwe na malengo na mpango wa kuyafanikisha,” alieleza Chobo.
Katika kikao hicho, watumishi kutoka kada za elimu, afya na kilimo walijadiliana kwa pamoja namna ya kuboresha utoaji huduma katika maeneo yao.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na wataalamu wa sekta ya elimu ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni ili kuboresha mahudhurio na kiwango cha ufaulu.

Vilevile kuongezeka kwa idadi ya walimu mashuleni, wakiwemo wa kujitolea, ili kupunguza msongamano wa madarasa.
Kwa upande wa sekta ya kilimo, wataalamu walimshauri Diwani kujikita katika kilimo cha kisasa chenye tija, hususan mazao ya biashara kama korosho na mazao ya chakula ili kuongeza uzalishaji na kujenga ustawi wa jamii.



