Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BENKI ya CRDB imeingia rasmi kati8ka makubaliano ya ushirikiano na Taasisi ya Aga Khan, makubaliano yanayolenga kurahisisha ulipaji wa ada na malipo mengine kwa shule zinazoendeshwa na taasisi hiyo hapa nchini.

Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Dar es Salaam katika hafla iliyowakutanisha viongozi wa taasisi zote mbili, ikiwa ni hatua kubwa inayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na usalama wa malipo kwa wazazi na walezi wa wanafunzi.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Rabala, alisema ushirikiano huo ni mfano bora wa jinsi sekta ya fedha inavyoweza kushirikiana na sekta ya elimu katika kuimarisha huduma na kuongeza thamani kwa jamii.

“Ushirikiano huu unaonyesha dhamira ya kweli ya Benki ya CRDB katika kuleta mageuzi ya huduma za kifedha kupitia ubunifu na ushirikiano wa kimkakati. Tunaamini hatua hii itaimarisha imani ya wazazi na kuleta ufanisi katika mfumo wa malipo kwenye shule za Aga Khan,” alisema Rabala.

Rabala aliongeza kuwa, katika kuadhimisha miaka 30 ya kutoa huduma kwa Watanzania, benki hiyo imeendelea kujikita katika kuhakikisha huduma zake zinagusa maisha ya watu kwa namna chanya, zikiwa na alama ya ubora na usalama wa hali ya juu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa CRDB, Gerald Kamugisha, alieleza kuwa benki hiyo imejipanga vyema kuhudumia shule zote za Aga Khan — kuanzia shule za awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu — katika maeneo yote nchini.

“Tumejipanga kupanua teknolojia ya kidijitali na kuhakikisha huduma zetu zinafika kwa haraka na kwa ufanisi kwa kila shule. Hili ni mojawapo ya matarajio yetu katika kuendeleza elimu kwa njia za kisasa,” alisema Kamugisha.

Naye Ofisa Mkuu wa Fedha wa Taasisi ya Aga Khan, Karim Munir, alieleza kuridhishwa kwake na ushirikiano huo, akiitaja Benki ya CRDB kuwa ni mshirika makini anayezingatia mahitaji ya wateja wake.

“Tunapongeza juhudi za CRDB na tunatarajia kushirikiana nao zaidi katika maeneo mengine ya kimkakati kwa maendeleo ya pamoja,” alisema Munir.

Makubaliano haya yanatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika urahisi wa ulipaji wa ada za shule, huku yakichochea matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali kwa manufaa ya walimu, wazazi na wanafunzi kote nchini.