Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BENKI ya CRDB imemkabidhi Rahabu Mwambene zawadi ya gari aina ya Ford Ranger XLT baada ya kushinda katika Droo ya tatu ya kampeni ya Tembocard ni Shwaa.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam ‘Sabasaba’, Afisa Mkuu wa Biashara wa CRDB, Boma Rabala, alisema kampeni hiyo imekuwa na mafanikio makubwa na imevuka matarajio ya benki hiyo, huku ikiendelea kuwahamasisha Watanzania kutumia kadi za CRDB kufanya miamala salama na rahisi.

“Leo tunayo furaha kubwa kwa kuwazawadia wateja wetu waliojitokeza kushiriki kampeni hii. Tunawapongeza washindi wetu wakubwa watano watakaoenda Ulaya kwa gharama zote kulipiwa na benki, pamoja na Rahabu Mwambene aliyeshinda gari jipya ambalo halijawahi kuendeshwa,” alisema Rabala.

Ameeleza kuwa CRDB itaendelea kumshika mkono Rahabu, ambaye ni mfanyabiashara mdogo wa kati, ili kumsaidia kufikia kiwango cha juu zaidi katika biashara yake. “Tunaahidi kushirikiana naye kumwezesha kuwa mjasiriamali mkubwa nchini,” aliongeza.

Kwa upande wake, Rahabu Mwambene ambaye huu ni mwaka wake wa 10 akiwa mteja wa CRDB, alisema alianza kutumia benki hiyo mwaka 2015 kwa shughuli zake za kibiashara, ikiwemo malipo ya mizigo ya nguo anazouza eneo la Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

“Mara ya kwanza walipopiga simu nilidhani ni matapeli, lakini nilipoenda tawi la CRDB walinithibitishia kuwa ni kweli. Nawashauri Watanzania waamini droo hizi ni za kweli, na kama huna kadi ya CRDB nenda kasajili,” alisema Rahabu kwa furaha.

Vivian Sinare, mmoja wa washindi wa zawadi za safari, naye alieleza kufurahi kwake na kuwahimiza wengine kuendelea kutumia huduma za benki hiyo.

CRDB imeahidi kuja na kampeni nyingine kubwa zaidi, baada ya mafanikio ya Tembocard ni Shwaa, huku matumizi ya huduma za kidigitali kama SimBanking yakiongezeka kwa kasi kutokana na kampeni hiyo.