Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KATIBU Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Makwiro, ameipongeza Benki ya CRDB kwa juhudi zake katika kuwawezesha wajasiriamali kupitia mafunzo ya teknolojia na matumizi ya mitandao ya kijamii katika kuendesha biashara.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wakati wa kufunga semina ya msimu wa tatu ya Instaprenyua, Makwiro alisema mafunzo hayo ni nyenzo muhimu katika zama hizi za mabadiliko ya kidijitali.

“Niwashukuru CRDB kwa kuja na wazo hili zuri la kuwashika mkono wajasiriamali wetu. Pia nawapongeza wale wote waliojitokeza kushiriki mafunzo haya. Kumbukeni maarifa ni mtaji mkubwa…siondoke hapa bila kupata kitu,” alisema Makwiro.

Alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia, hususan mitandao ya kijamii na simu za mkononi, yamebadilisha kabisa namna biashara zinavyoendeshwa, hivyo kuwapa wajasiriamali nafasi adhimu ya kufikia masoko mapya na kuongeza tija.

Alibainisha, kwa mujibu wa takwimu kutoka hotuba ya bajeti ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka hadi milioni 90 kufikia Aprili 2025, huku watumiaji wa intaneti wakifikia milioni 49 ongezeko la asilimia 32 kutoka mwaka uliopita.

“Niwapongeze CRDB kwani kwa kuandaa mafunzo haya, mnalenga watu zaidi ya milioni 49 wanaotumia huduma za intaneti nchini. Hii ni fursa kubwa kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali,” aliongeza.

Hata hivyo, aliwahimiza wajasiriamali kuwa makini na matumizi ya mitandao, akitaja kuwa kulikuwa na zaidi ya majaribio 11,700 ya ulaghai mtandaoni katika robo ya kwanza ya mwaka huu pekee, huku mikoa ya Rukwa na Morogoro ikiongoza kwa visa hivyo.

Makwiro pia alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuimarisha miundombinu ya kidijitali, ikiwa ni pamoja na kuunganisha Wilaya na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Hadi sasa, Wilaya 109 kati ya 139 zimeunganishwa, hatua itakayochochea biashara mtandaoni kwa kasi zaidi.

Katika uzinduzi wa semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema semina ya Instaprenyua ambayo sasa ipo kwenye msimu wake wa tatu inalenga kuwajengea uwezo wafanyabiashara wadogo na wa kati kutumia teknolojia kukuza biashara zao.

“Ujasiriamali wa mtandaoni hauhitaji kuwa na followers wengi pekee. Unahitaji maarifa sahihi, mbinu za kisasa, ubunifu, nidhamu ya kifedha na uwezo wa kutumia taarifa kufanya maamuzi bora ya kibiashara,” alisema Nsekela.

Alitoa wito kwa washiriki kutumia maarifa waliyopata kuboresha biashara zao na kuwa mfano wa mabadiliko katika jamii.

Alifafanua kuwa, kwa sasa zaidi ya asilimia 95 ya huduma za CRDB zinafanyika kidijitali kupitia mifumo kama SimBanking, TemboCard, na Lipa Hapa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kukidhi mahitaji ya soko la kisasa.

“Benki hii pia imeanzisha huduma maalum kwa ajili ya wajasiriamali ikiwemo KOMBOA LOAN, Akaunti ya Hodari, na misaada ya mitaji kupitia CRDB Bank Foundation, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anayebaki nyuma kwenye mapinduzi ya kidijitali,” alisema.

Kupitia semina hiyo, wajasiriamali walijifunza matumizi ya zana muhimu kama SEO, funnels, hashtags, na maudhui ya kuvutia kupitia majukwaa kama TikTok, Instagram Reels na WhatsApp Business.

Pia, walipata mafunzo ya kulinda biashara dhidi ya matapeli wa mtandaoni na kutumia takwimu kufanikisha kampeni za kidijitali.