Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BENKI ya CRDB imezindua rasmi huduma mpya ya kidijitali inayojulikana kama Tokenization, itakayowawezesha Watanzania wakiwemo wale wasiokuwa na akaunti ya benki kupokea fedha kutoka kwa mawakala wa CRDB bila kutozwa gharama ya ziada.

Uzinduzi wa huduma hiyo umefanyika leo Oktoba 13, 2025 jijini Dar es Salaam, ukiongozwa na Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam wa Benki ya CRDB, Muhimuliza Buberwa, katika kongamano lililowakutanisha zaidi ya mawakala 800 wa benki hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Buberwa amesema kuwa huduma ya Tokenization inalenga kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini kwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za kifedha bila kujali kama ana akaunti ya benki au la.

“Kupitia Tokenization, mteja anaweza kutuma au kupokea fedha kwa urahisi kupitia mawakala wetu bila kulazimika kuwa na akaunti. Hii ni njia salama, ya haraka na rafiki kwa wote,” amesema Buberwa.

Ameongeza kuwa huduma hiyo imejengwa kwenye mfumo salama wa kidijitali unaorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa njia ya kisasa, salama na isiyo na vikwazo vya kimfumo, sambamba na mkakati wa benki hiyo wa kuboresha teknolojia na ubunifu katika huduma za kifedha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawakala na Huduma za Malipo wa CRDB, Catherine Lutenge, amesema semina hiyo imeandaliwa kwa ajili ya kuwawezesha mawakala kutoa huduma kwa ufanisi zaidi kupitia mafunzo ya matumizi ya mashine za POS na teknolojia mpya ikiwemo Tokenization.

“Tunataka mawakala wetu waende sambamba na mabadiliko ya kidijitali. Mafunzo haya yatawawezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wetu popote walipo,” amesema Lutenge.

Lutenge ameongeza kuwa huduma hiyo itasaidia pia katika kuongeza mzunguko wa fedha katika maeneo ya vijijini, jambo litakalosaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.