Na Mwandishi Wetu, JammhuriMedia, Dar es Salaam

SHIRIKISHO la Wenye Viwanda Nchini (CTI), limesema ushirikiano mzuri baina ya serikali na shirikisho hilo umechangia kwa kiwango kikubwa kutatua changamoto mbalimbali zzilizokuwa zikiwakabili wenye viwanda.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Mhandisi Benedict Lema, wakati akizungumza kwenye ziara ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga kwenye viwanda mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Lema alisema CTI na wenye viwanda nchini wanathamini uhusiano mzuri uliopo baina ya serikali na wenye viwanda ambao umekuwa na manufaa makubwa kwenye kutatua changamoto zao.

“Kuna uhusiano wa karibu sana baina ya ofisi ya Waziri wa Viwanda na CTI, ushirikiano huu ndio unafanya wawekezaji kuwa na mori wa kufanya zaidi na kutimiza malengo ya serikali yetu, mheshimiwa Waziri ziara yako yaa leo ni uthibitisho wa kutosha tosha kuonyesha uhusiano mwema baina ya ofisi yako na wazalishaji wa viwandani,” alisema

Alisema viwanda vinatekeleza ajenda ya serikali kwa kuongeza ajira kwa vijana na kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi wan chi kutokana na kodi zinazolipwa na wenye viwanda.

“Mheshimiwa Waziri ulipoteuliwa tu ulitembelea CTI na tuliufurahi sana kwasababu tulikueleza ya kwetu ambayo sisi tunaamini utayatekeleza kwa maslahi ya nchi yetu,” alisema.

Naye Waziri wa Viwanda, Judith Kapinga alisema lengo la ziara hiyo ni kuwahakikishia wenye viwanda ushirikiano wa kutosha kuhakikisha wanaendelea kuzalisha kwa wingi na kutengeneza ajira zaidi kwa watanzania.

Waziri alisema nia ya serikali ni kutengeneza ajira mpya 8,000,000 mpaka kufikia mwaka 2030 hivyo itaendelea kuwawekea mazingira mazuri wenye viwanda ili waongeze uzalishaji.

“Alipoapishwa Rais Samia aliahidi kuwa ndani ya siku 100 atahakikisha ajira za vijana zinaongezeka ndiyo maana tutaendelea kuwasaidia ili muongeze uzalishaji na kuongeza ajira kwa vijana, nyinyi ALAF mnachukua vijana ambao hawana ujuzi wa kutosha mnawapa mafunzo na kisha mnawapa ajira, hilo ni jambo jema sana,” alisema

“Teknolojia inakuwa siku hadi siku kwa hiyo nasisi serikali imeshabadilisha mitaala kuhakikisha inaendana na soko la ajira na katika hilo tumedhamiria kufikia ajira milioni nane mpaka kufikia mwaka 2020,” alisema Kapinga.