Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini, Othman Dunga ameeleza kuwa CUF haishiriki uchaguzi kwa ajili ya kushiriki tu, bali kwa lengo la kushinda na kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi.
Ameeleza kuwa Watanzania wamechoshwa na ahadi zisizotekelezeka kutoka kwa viongozi waliopo madarakani tangu nchi ipate uhuru, hali inayowafanya wananchi wengi kupoteza matumaini na kuhisi hawana pa kukimbilia
“Uchaguzi huu ni fursa ya kipekee kwa wananchi wa Kondoa na Watanzania kwa ujumla kufanya maamuzi sahihi kwa kuchagua viongozi wanaojali maslahi yao.
“Sisi tumeweka mgombea wa Urais makini na ambaye tunajua ataibuka mshindi kwa kuwa tumejipanga kuzunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi kwanini wanatakiwa kutuchagua,” amesema Dunga.
Aidha amesisitiza umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi isiyoegemea upande wowote wa kisiasa, pamoja na kuhakikisha kuwa TAKUKURU inachukua hatua kali dhidi ya wote watakaohusika na vitendo vya rushwa na uvunjaji wa maadili ya uchaguzi.
“Tunaitahadharisha Tume ya Uchaguzi kuacha kupendelea vyama fulani na isithubutu kutangaza washindi wa uongo,Tunataka haki itendeke na matokeo ya uchaguzi yaakisi maamuzi ya wananchi,” aliongeza.
Kuhusu Jimbo la klKondoa Dunga amesema kuwa pamoja na kuwa na mbunge ambaye alipata kuwa waziri, bado hakuna maendeleo ya maana yaliyowafikia wananchi wa Kondoa.
“Ninakwenda kutatua changamoto zote zinazowakabili wananchi wa Kondoa ni wakulima kwa asilimia 90 lakini hawana soko la uhakika la kuuza mazao yao.
“Nitahakikisha kuwa wanapata masoko ya moja kwa moja na nitafuta mfumo wa ‘stakabadhi ghalani’ unaowanyima wakulima uhuru wa kuuza mazao kwa bei wanayoitaka,” amesema.
Aidha ameahidi pia kuboresha miundombinu ya barabara, kutengeneza fursa za ajira kwa vijana, na kuhakikisha upatikanaji wa mikopo kwa wanawake.
Kuhusu Hifadhi ya Mkongonero Game Reserve, Dunga ameeleza kuwa mipaka yake imesogea na kuvamia makazi ya watu, jambo ambalo halikubaliki.
“Hivyo nitahakikisha mpaka huo unarudishwa nyuma kwa umbali unaostahili ili wananchi wapate nafasi ya kuishi kwa amani, bila kugombea maeneo na wanyama, ni lazima tuwe na uwiano kati ya hifadhi na haki za binadamu,” amefafanua
Katika hatua nyingine Dunga ameeleza kuwa anakwenda kutafuta majibu ya changamoto zote zinazowakabili wananchi wa Kondoa kwa kuwaletea maendeleo ya kweli.
