Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo, amewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kupiga kura, akisisitiza kuwa ndio njia  pekee itakayowezesha kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Pia mgombea urais huyo ameitaka Tume Huru ya Uchaguzi kutenda haki na usawa kwa vyama vyote katika kusimamia uchaguzi  ikiwa ni pamoja na kuvitaka vyombo vya dola kutoegemea upande chama chochote badala yake haki ikatendeke. 

Mgombea urais huyo ametoa rai hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma ambapo ameeleza kuwa msimamo wa chama hicho ni kushiriki ipasavyo katika uchaguzi mkuu. 

“Sasa hivi nasikia watu wanahamasishana kule tarehe 29 tusiende kupiga kura sijui nini na nini msijidanganye CUF hii iliwahi kususia uchaguzi Zanzibar Jecha alifuta uchaguzi wakasusia kwenda CCM wakashangilia kwamba ukisusa wenzio wala wanasema hivyo wakashangilia kabisa, “alisisitiza Gombo

“Jamani eeh vita vizuri kavipigane humo ndani hakuna kususa mtu hapa nendeni mkapige kura siku ikifika na wala asikose mtu na mzilinde na kura zenu kwa kuwa kura zenu zipo na zitakaa salama usisuse kwani unasusa nini usipokwenda kuchagua utachaguliwa yule usiyempenda halafu tena urudi kulalamika, “alisema Gombo. 

Katika hatua nyingine Gombo amesema kwamba iwapo atapata ridhaa ya kuwa Rais atakahakikisha huduma zote za afya zinatolewa bure kwa watanzania wote.