Mgombea wa ubunge katika Jimbo la Morogoro Mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Nyambi Athuman amesema kuwa vipaumbele vya ilani ya chama hicho ni kutokomeza umasikini kwa kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia vikundi vya uzalishaji mali kama SACCOS.

Pia ni kuboresha huduma jumuishi za kifedha, kupanua ajira nadhifu kupitia programu za kilimo, biashara ndogo za kazi na viwanda vidogo na kuanzisha mpango wa ruzuku ya huduma za msingi kwa familia masikini.

Akizungumzia ilani ya CUF, mgombea huyo alitaja vipaumbele vingine ni kutokomeza njaa, pembejeo za kisasa kwa wakulima, kukuza kilimo endelevu, uboreshaji wa huduma za ugani, kilimo cha umwagiliaji, maeneo ya mabonde, masoko ya uhakika ya mazao kwa wakulima kupitia ushirika na mifumo ya kidijitali.

Alisema CUF katika falsafa ya Haki Sawa kwa Wote, inahakikisha kila mwananchi anapata haki zake za kiuchumi, kijamii, mazingira bora na kipato cha msingi.

Athuman alisema kupitia Ilani hiyo ya uchaguzi ya mwaka huu, CUF inalenga kuongoza kwa uadilifu, ufanisi na ushirikishwaji wa wananchi katika kila hatua ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Alisema ilani hiyo imeweka kipaumbele kuboresha afya njema na ustawi wa jamii, elimu bora na jumuishi, kusimamia usawa wa kijinsia na haki za kundi maalumu.

Alitaja eneo lingine ni kuwezesha wananchi kupata nishati safi ya kupikia, kuongeza matumizi ya umeme wa jua kwenye shule, vituo vya afya na mitaa ya pembezoni iliyopo kwenye jimbo hilo.