Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza

Chama cha Wananchi CUF, kimesema endapo kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi kitahakisha kinatoa huduma ya matibabu bure kwa wananchi wote katika hospitali za Serikali.

Pamoja na kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya awali mpaka chuo kikuu(elimu ya juu), ili kutoa fursa kwa watanzania wote kupata haki ya elimu na kuwa na taifa bora lenye wataalamu wengi.

Hayo yamebainishwa na mgombea urais kupitia chama cha Wananchi CUF,Gombo Samandito Gombo,wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza kuelekea uzinduzi wa kampeni ya chama hicho,unaotarajia kufanyika Agosti 31, mwaka huu uwanja wa Furahisha  wilayani Ilemela mkoani.

Ambapo amesema  sera ya chama hicho ni haki  sawa kwa wote na kinataka kila mtu awe na furaha huku akutaja vipaumbele   10 endapo chama hicho kitapewa ridhaa katika uchaguzi mkuu.

Amesema mara baada ya kuapishwa kuwa rais  jambo la kwanza ni kutoa matibabu bure kwa wananchi kwani ni wajibu wa Serikali kufanya hivyo.

“Sisi chama cha wananchi CUF hatuamini katika bima ya afya kwa sababu tumeku nayo kwa muda mrefu lakini utendaji kazi wake siyo mzuri,imekuwa  chanzo cha rushwa na ubadilifu wa fedha,tunayo rasilimali ya kutosha kama nchi ya kuweza  kuwahudumia wananchi wetu bila ya kutoa malipo ya aina yoyote kwenye huduma zetu za afya,”amesema Gombo na kuongeza:

“Wananchi wakitupa ridhaa Oktoba,matibabu yatakuwa bure kuanzia siku hiyo nitakapo maliza kuapa kama Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania,kuanzia mwanzo,Bugando hadi Muhimbili kote  kwenye hospitali  za Serikali hakutakuwa na bima ya afya,”.

“Huduma ya afya ni jambo la msingi na kila Mtanzania anatakiwa alipate bila kujiuliza uliza,kwa sababu katika maisha ya binadamu  dharura kubwa uwa ni afya,mambo mengine yanaweza kujitokeza mfano  ukitaka kuoa  ukasema nimeshindwa kuoa kwa sababu sina mahari ya kutosha,nitaoa mwakani ukahairisha.Lakini unapoanza kuumwa uwezi kuhairisha kwenda kutibiwa,siyo kila mtu ana uwezo wa kulipa na ni jukumu la Serikali kuhakikisha kila mtu anapata huduma ya afya,”.

Pia amesema,chama hicho kikipats ridhaa kinataka huduma ya msingi kama elimu itolewe bure kuanzia ngazi ya awali mpaka chuo kikuu.

“Elimu ni haki ya msingi ya binadamu na kwa bahati nzuri Tanzania tunazo rasilimali nyingi za kutosha kuhakikisha watoto wetu wanasoma bila kuambiwa lipa hiki mara hiki.Kwa sababu mali zilizopo ni za watanzania wote,”amesema Gombo.

Hata hivyo amesema endapo CUF itashika madaraka suala la kupotea watu halitakuwepo kwani litahakikisha vyombo vya dola vinafanya kazi yake kwa ufasaha kwa kuendelea kulinda wananchi na kuishi katika usalama.

Aidha amesema, kila mfanyakazi wa umma atapatiwa hati ya kiwanja, pamoja na mkopo nafuu wa kujengewa nyumba na kupewa gari ili kupunguza masuala ya rushwa watumushi wa umma.