Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

MKUU wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali, amekipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini, akieleza kuwa chuo hicho kina nafasi ya kipekee nchini.

Akizungumza alipotembelea banda la UDSM katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji kitaifa (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, Machali amesema amevutiwa sana na teknolojia mbalimbali zinazobuniwa na wanafunzi na watafiti wa chuo hicho.

“Tumewaona mabinti wadogo kabisa wakitengeneza bidhaa za thamani kama mafuta yanayosaidia kuondoa makunyanzi. Hii inaonyesha namna ambavyo UDSM imewekeza kwenye ubunifu wa vitendo,” amesema Machali.

Ameongeza pia amejionea teknolojia ya kisasa katika sekta ya ufugaji wa samaki, ikiwemo mashine ya kukamata vifaranga bila kutumia mikono, ambayo inapunguza vifo vya vifaranga kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na njia za kawaida.

“Kwa mujibu wa wataalam, kutumia mikono kuna hatarisha maisha ya vifaranga kwa zaidi ya asilimia 25, lakini kwa kutumia mashine hiyo ni nadra sana vifaranga kufa,” amebainisha.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuwaalika wazalishaji wa vifaranga nchini kutembelea banda la UDSM ili kujifunza zaidi kuhusu teknolojia hizo, akisisitiza kuwa zitawasaidia kuboresha uzalishaji na kupunguza hasara.

Katika hatua nyingine, amesifu maendeleo ya kidijitali yanayofanywa na UDSM kupitia programu za simu (apps) zinazowaunganisha wakulima moja kwa moja na watoa huduma za kilimo, jambo ambalo linapunguza hitaji la safari ndefu za kwenda ofisini kwa maafisa kilimo.

“Hii ni fursa kubwa kwa wakulima wetu. Kupitia apps hizi, mkulima anaweza kupata huduma zote za kilimo akiwa kijijini kwake bila kuhangaika,” aliongeza.

Machali ameipongeza UDSM kupitia Ndaki ya Masuala ya Kilimo na Teknolojia zake kwa jitihada kubwa na mchango wao kwa maendeleo ya Taifa.