Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, ametoa rai kwa walimu na wasimamizi wa shule kuwatambua na kuwafuatilia wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto za kijamii.
Amesisitiza kuwa uwekezaji wa miundombinu ya elimu hautakuwa na matokeo chanya bila ustawi wa mwanafunzi mmoja mmoja.
Nickson alitoa wito huo leo Januari 26, 2026 wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa madawati, viti na meza zenye thamani ya sh. milioni 400 kwa shule za msingi na sekondari za Manispaa ya Kibaha, tukio lililofanyika katika Shule ya Msingi Mkoani.
“Wakati Serikali na wadau wakiendelea kuboresha mazingira ya shule, bado kuna wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu, wanaofanyiwa unyanyasaji, wasio na malezi salama au wanaokosa msaada wa kisaikolojia, hali inayoweza kuathiri maendeleo yao ya kielimu “
“Tumewekeza katika miundombinu, lakini sasa ni lazima tujue watoto wetu wanatoka wapi, wanaishi mazingira gani na wanapitia changamoto zipi, tukiwatambua mapema, tutawawezesha na kuinua taaluma zao,” alifafanua Nickson.
Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, alisema idadi ya wanafunzi imeendelea kuongezeka kila mwaka, akibainisha kuwa shule za sekondari kulikuwa na wanafunzi 19,606 mwaka 2025 hadi 22,138 mwaka 2026, huku shule za msingi zikiongezeka kutoka wanafunzi 44,128 hadi 46,324.
Alisisitiza kuwa hakuna mwanafunzi atakayekaa chini, akiwataka wakuu wa shule kusimamia na kutunza madawati hayo ili yadumu kwa muda mrefu .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, alisema utengenezaji wa madawati ulianza Novemba 12, 2025 na kukamilika Machi 29, 2026 kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya Manispaa.
Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Mwajuma Nyamka, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulinda heshima ya Taifa na kuisimamia Tanzania katika misingi ya amani pamoja na kuboresha sekta ya elimu.







