Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

MKUU wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, amesema migogoro mikubwa ya ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha imedhibitiwa, huku baadhi ya migogoro ya mipaka ikiwasilishwa katika mamlaka husika ili kuhakikisha wananchi hawaathiriki katika upatikanaji wa huduma za kijamii .

Nickson ametoa wito kwa viongozi kuanzia vitongoji hadi kata kufanya kazi kwa utashi ili kupunguza makali miongoni mwa wananchi, hususan kwa upande ambao haukuridhishwa na maamuzi ya kisheria katika utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Akizungumza katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, kufuatia hoja ya Diwani wa Kata ya Kikongo, Halima Jongo, kuhusu malalamiko yaliyoibuka baada ya maamuzi ya Tume ya Uchunguzi pamoja na Waziri wa Ardhi kumpa haki mwekezaji na mmiliki halali wa eneo la Lupunga, Kikongo, TARIQ, Nickson aliwataka viongozi kufanya kazi kwa utashi kwa kutoa elimu kwa jamii.

“Palipo na migogoro ya ardhi huwa kuna pande mbili, na katika utatuzi wa kisheria kuna anayepata haki na anayeshindwa, Waliokosa mara nyingi huzalisha malalamiko katika ngazi mbalimbali za maamuzi,” alifafanua Nickson.

Aliwataka pia viongozi kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na kuwasaidia wanaohitaji msaada, huku akisisitiza kuwa uongozi ni dhamana ya kuwaletea wananchi maendeleo na utulivu.

Aidha, Nickson aliwaasa madiwani kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisema diwani atakayejitokeza kuwa kinara katika kusukuma mbele maendeleo atapatiwa zawadi kama motisha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Regina Bieda, alisema mgogoro wa eneo la Lupunga, Kikongo, umepitia hatua zote za kisheria ikiwemo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Tume ya Uchunguzi, ambazo zilitoa maamuzi kuwa mmiliki halali wa eneo hilo ni TARIQ, huku wananchi waliovamia eneo hilo wakitakiwa kuondoka.

Regina aliwaasa watendaji na madiwani kuheshimu na kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya Serikali, akisisitiza kuwa wao kama watekelezaji wanapaswa kufuata itifaki na maelekezo yanayotolewa, sambamba na kuwapa wananchi ushauri wa kitaalamu pale inapohitajika.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Soga, Shomari Mwinshehe, alisema wamepokea maelekezo ya Mkuu wa Wilaya na kuyataja kuwa ni ya kujenga na yenye lengo la kuimarisha utendaji kazi.

Kuhusu kero ya mamba katika Mto Ruvu, Shomari alisema Idara ya Maliasili na Mazingira tayari imeanza zoezi la kuvuna na kuwaondoa mamba hao ili kupunguza kero na hatari kwa wananchi wanaoishi maeneo ya jirani.