Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mirerani
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara, Fakii Raphael Lulandala ameagiza watu wanaoishi mabondeni katika tarafa ya Moipo wahame mara moja ili kuepuka madhara ya mafuriko yanayosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Lulandala ametoa agizo hilo baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Tarafa ya Moipo yaliyokumbwa na mafuriko na kutoa pole kwao.
Lulandala amewaasa waliopo mabondeni katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko kuhama ili kuondokana na adha hiyo ya makazi yao kuzingirwa na maji.
Amesema siyo busara watu kuendelea kuishi katika nyumba zilizozungukwa na maji ilihali bado mvua zinaendelea kunyesha.
“Huu ni wakati wa kujibanza kwa ndugu na jamaa kuliko kuendelea kuishi katika maeneo ya mabondeni huku mvua zikiendelea kunyesha na kusababisha mafuriko,” amesema Lulandala.
Hata hivyo, ameagiza taasisi za serikali za eneo hilo, kuwapokea wahanga wa mafuriko hayo ili waweze kuishi wakati huu wakipambana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kunyesha.
Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Laizer amesema ekari 10,000 za mazao ya mahindi na maharage iliyokuwa imepandwa mashambani ikisubiriwa kuota imesombwa na mafuriko.
Taiko amesema mazao hayo yalikuwa yamepandwa na wakulima mashambani ila maji yaliyotokana na mafuriko yamewapa hasara wakulima.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kairo kata ya Endiamtu, Gadi Msuya amesema mafuriko yamewakumba baadhi ya wakazi wa eneo hilo na wengine makazi yao kuingiliwa na maji.
Mkazi wa mtaa wa Kangaroo kata ya Mirerani Mwajuma Idd amesema maji yameingia katia nyumba yao na mengine yamezingira makazi yao.


