Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetoa onyo dhidi ya watu wote wanaotangaza, kuhamasisha au kusifia matumizi ya dawa za kulevya kupitia nyimbo, mavazi na njia nyingine yoyote ya sanaa na mawasiliano, huku ikisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (SabaSaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam, baada ya kutembelea.

“Hatutasita kuchukua hatua kali kwa yeyote anayepotosha jamii, hasa vijana, kwa njia ya kusifia au kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya kupitia nyimbo, mavazi au kazi yoyote ya sanaa. Huu ni uhalifu kama mwingine wowote na tutawafikisha kwenye mkono wa sheria.
“Watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya iwe ni kuzalisha, kusambaza au kutumia wanapaswa kuacha mara moja kwani mkono wa chuma utawafikia na pumzi ya moto itawaelekea,” amesisitiza.
Kamishna Lyimo pia aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawalea watoto wao katika misingi ya maadili na kuwaepusha na vishawishi vinavyoweza kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya, akisisitiza kuwa taifa linahitaji kizazi chenye afya bora kwa ajili ya kujenga uchumi imara na endelevu.
Akizungumzia hali ya vita dhidi ya mihadarati nchini, Kamishna Lyimo alisema mafanikio yanaendelea kuonekana kutokana na operesheni mbalimbali zinazofanyika na juhudi za kuwapeleka waraibu waliopatwa na madhara ya dawa hizo kwenye vituo vya tiba kwa ajili ya matibabu yanayotolewa bure na serikali.

“Takwimu zinaonesha kuwa upatikanaji wa dawa kama heroini na cocaine umepungua kwa kiwango kikubwa. Kwa sasa, hata kwenye vijiwe ambavyo zamani dawa hizi zilikuwa zikisambazwa, hazipatikani tena,” alisema.
Kwa upande wa maonesho ya Sabasaba, DCEA imekuwa ikitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu aina za dawa za kulevya, madhara yake na sheria zinazoongoza mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.
“Tupo katika operesheni maalum ya kutoa elimu nchi nzima kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo. Wakati huo huo, tunafanya operesheni ya kuwakamata wale wote wanaoendelea kujihusisha na biashara hii haramu,” alifafanua Kamishna Lyimo.

Akimhitimisha hotuba yake, Kamishna Jenerali Lyimo alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na afya bora ili kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.
“Vita hii si ya serikali pekee. Ni vita ya taifa zima. Kila mmoja anapaswa kuwa askari katika kuhakikisha tunatokomeza dawa za kulevya kabisa nchini,” alihitimisha.