Na Byarugaba Innocent, JamhuriMedia, Nyasa DC

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Khalid Khalif ameendelea na utaratibu wake wa kawaida wa kuwatembelea wakandarasi kwenye Kandarasi za Miradi ya Maendeleo inayoendelea kutekelezwa ikiwa ni sehemu ya kuhimiza ukamilishwaji kwa wakati na ubora unaoendana na thamani ya fedha inayotumika.

Khalif akiwa ameambatana na Wataalam kutoka divisheni ya Ujenzi, Mipango na uratibu m na Afya wametembelea Miradi yenye thamani ya Shilingi 582,017,569 ya Sekta ya Afya na Elimu ambayo utekelezaji wake upo katika hatua tofauti kwa lengo la kuwahimiza wakandarasi kuongeza kasi ya kukamilisha miradi kwa wakati ili iweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Miradi iliyotembelewa ni ujenzi wa madarasa 2, Vyoo matundu 6 na Madawati 30 shule ya Msingi Chiulu yenye thamani ya shilingi 58,200,000 ukamilishaji wa jengo la utawala shule ya Sekondari Unberkant Shilingi 50,000,000 ujenzi wa bwalo la chakula, madarasa 2, Vyoo matundu 8 na ununuzi wa viti 60,Meza 60 shule ya Sekondari Nyasa shilingi 223,817,569 kwa upande wa Sekta ya Elimu huku Sekta ya afya ukitembelewa mradi wa Ujenzi wa Kituo cha afya Chiwanda kitakachogharimu Shilingi 250,000,000 na kuhudumia wananchi 9691 kutoka vijiji vya Kwambe, Chimate, Mtupale na Ngombo ukiwa katika hatua za awali.

Khalif amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia fedha nyingi Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa zinazolenga kuboresha sekta zote ikiwemo Afya na Elimu.

Aidha,ametoa rai kwa wakandarasi kukamilisha miradi kwa wakati ili wananchi waendelee kunufaika na matunda ya Kodi yao na kwamba mkandarasi atakayechelewesha mradi ama Kujenga chini ya kiwango atakumbana na rungu la sheria kwa mujibu wa taratibu.

Evelyne Mwakibete Mratibu wa Miradi, Miriam Panja Mchumi na Mhandisi Allen Mshiu wamesema wataendelea kutoa ushauri wa kitaalam wa kifedha na kihandisi kwa wakandarasi ili kuhakikisha kuwa Miradi inakamikika kwa wakati na ubora unaolingana na thamani ya fedha.