Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, amesema Serikali ipo kwenye hatua za mwisho kukamilisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, mpango kabambe wa muda mrefu utakaotoa mwelekeo wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi
Kwa ujumla, Dira ya Maendeleo 2050 inalenga kuipambanua Tanzania kama taifa shindani, jumuishi, lenye ustahimilivu wa kiuchumi, ambapo kila mdau wa maendeleo, kutoka sekta ya umma hadi binafsi, anashiriki kikamilifu kufanikisha maono ya pamoja.

Akizungumza Juni 19, 2025 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Dkt. Kida ameeleza kuwa rasimu ya Dira hiyo itatowasilishwa Bungeni Juni 26, 2025, na endapo itapitishwa, itazinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kazi kubwa ya ofisi yetu kwa sasa ni kukamilisha maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Itakapopitishwa na Bunge, itakuwa dira rasmi ya nchi kwa miongo ijayo,” amesema Dkt. Kida.
Ameeleza kuwa Dira hiyo itaambatana na mpango wa utekelezaji wa muda mrefu, utakaoeleza kwa kina namna ambavyo Serikali itatekeleza maono makuu yaliyomo katika Dira hiyo kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kulifikisha taifa katika uchumi wa thamani ya trilioni moja.
“Tunahitaji dira yenye mwelekeo wa kweli, lakini pia mpango mahsusi wa utekelezaji. Hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha tunapata matokeo yanayotarajiwa,” ameongeza.

Kwa upande wake Mchumi wa Ofisi hiyo
Octavian Ruta amesisitiza ushiriki wa sekta binafsi hususan wawekezaji wa ndani ambapo ameeleza kuwa ndiyo nguzo kuu ya kufanikisha ndoto ya uchumi imara wa 2050.
Amesema sera ya uwekezaji imeboreshwa ili kumpa nafasi mwekezaji kwa misingi ya uwezo wake wa uzalishaji na mchango katika ajira, bila kujali uraia wake.
“Tunahitaji sekta binafsi, hasa wawekezaji wa ndani, waongeze kasi ya kuwekeza. Serikali imeweka mazingira wezeshi; sasa tunahitaji kuona matokeo,” amesema.
Kwa upande wa ushiriki wa wananchi katika maonesho hayo, Ruta amesena mwitikio ni mkubwa akibainisha kuwa zaidi ya wananchi 100 wametembelea banda la ofisi hiyo kwa lengo la kupata elimu kuhusu majukumu mapya ya ofisi hiyo pamoja na mwelekeo wa mipango ya muda mrefu.

“Ni dhahiri kuwa wananchi wanapenda kuelewa mpango wa muda mrefu wa nchi yao. Huu ni mwanzo mzuri wa ujenzi wa umiliki wa Dira ya 2050 miongoni mwa Watanzania,” amesema.
Katika hatua nyingine,amesema kuwa ofisi hiyo imeimarisha huduma za elimu ya moja kwa moja kwa wananchi kupitia Kliniki za Papo kwa Hapo, zinazowawezesha kupata maelezo na ushauri kutoka kwa wataalam wa masuala ya mipango na uwekezaji.
“Tunajenga msingi wa taifa linalojielewa, linalopanga kwa weledi, na linalohusisha wananchi katika kila hatua ya maendeleo,” amesema

