Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza imeanzisha kozi mpya zinazolenga kuongeza ujuzi wa vijana katika sekta ya ngozi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuchochea ajira na kuendeleza viwanda vidogo na vya kati nchini.
Akizungumza katika banda lao lililopo katika Viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba), Mkufunzi wa DIT Mwanza, Sharif Mwangi amesema taasisi hiyo sasa inatoa kozi ya Teknolojia ya Uchakataji Ngozi pamoja na kozi ya Teknolojia ya Bidhaa za Ngozi. Kozi hizo zimejikita katika mnyororo mzima wa thamani wa ngozi, kuanzia hatua ya kuchuna mnyama hadi kutengeneza bidhaa mbalimbali.

“Tunawafundisha vijana mbinu bora za kuchakata ngozi pamoja na kutengeneza bidhaa tofauti kama vile mikoba, mabegi, pochi (wallet), na hata mipira. Pia tunatoa huduma kwa wajasiriamali wanaotuletea ngozi kutoka nje ya taasisi, tunazichakata na wao huzitumia kutengeneza bidhaa,” amesema Mwangi.
Amesema ngozi zinazotumika katika mafunzo hayo zinatoka kwa wanyama tofauti wakiwemo mbuzi, ng’ombe, nyoka na samaki, na kozi hiyo ya miaka mitatu inahitaji mwanafunzi awe na ufaulu wa angalau D nne, ikiwemo masomo ya Hisabati, Fizikia na Kemia.
“Kozi hii inahusisha utaalamu wa uchakataji ngozi, maarifa ya kisayansi juu ya ngozi, na mbinu mbalimbali za kupata matokeo tofauti kulingana na matumizi ya bidhaa inayokusudiwa,” amefafanua.
Mbali na kozi ya miaka mitatu, DIT Mwanza pia inatoa mafunzo ya muda mfupi ya wiki nane kwa wajasiriamali wasiokidhi vigezo vya kujiunga na kozi rasmi, ili kuwapa maarifa ya msingi ya uchakataji na utengenezaji bidhaa za ngozi.
“Natoa wito kwa vijana na wanafunzi kujiunga na DIT ili wapate ujuzi utakaowasaidia kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa. Sisi tunafundisha kwa mtazamo wa ujasiriamali,” amesema.
Aidha, Mwangi amesema DIT ina mpango wa kufuatilia wahitimu wake ili kufahamu changamoto wanazokumbana nazo katika soko la ajira na namna bora ya kuwasaidia kupitia mipango ya maendeleo ya kitaasisi.

“Tuna malighafi nyingi nchini lakini bado hatujaweza kuzitumia ipasavyo kwa sababu ya ukosefu wa elimu na ujuzi. Ndio maana DIT tumeamua kutoa kozi hii, tumeanza hapa Mwanza kwa lengo la kuonesha njia,” amesisitiza.
Ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwasisitiza watoto wao kujiunga na kozi hizo, akisisitiza kuwa elimu hiyo inalenga kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kiuchumi kupitia ubunifu na ujasiriamali.