Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Masasi

Mbunge wa Jimbo la Masasi ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amekabidhi baiskeli kumi kwa watu wenye ulemavu wilayani Masasi mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kusaidia watu wenye mahitaji maalum katika jimbo hilo.

Dkt. Akwilapo amekabidhi baiskeli hizo Machi 8, 2026 wakati wa ziara yake mkoani Mtwara, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kurahisisha usafiri na shughuli za kila siku kwa watu wenye ulemavu ili waweze kujitegemea kiuchumi.

Amesema ari yake ya kusaidia watu wenye ulemavu imetokana na uzoefu wake wa maisha ya kulea mtoto mwenye ulemavu, jambo lililompa uelewa wa karibu kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo na umuhimu wa kuwasaidia.

Amebainisha kuwa, kusaidia watu wenye uhitaji ni jukumu la kila mwenye uwezo katika jamii, na kwamba ataendelea kuwahamasisha marafiki na ndugu kushiriki katika kutoa msaada kwa watu wenye uhitaji ili kuwapa furaha na matumaini.

“Mheshimiwa Rais Mama Samia alishatuambia kuwa katika kazi tunazofanya tuhakikishe tunawapa wananchi furaha.’’ amesema Dkt. Akwilapo.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa Masasi, msaada kwa watu wenye uhitaji unaweza kuwa mdogo au mkubwa kulingana na uwezo wa mtu, lakini jambo muhimu ni kushirikiana katika kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.

“Tutawaangalia watu wa madaraja yote, rika zote na wenye uwezo wowote ili kuwainua wale wenye uhitaji. Kimsingi tunataka wote tufikie hatua ya kuweza kuona fursa zilizo mbele yetu,” ameongeza.

Kwa upande wake, mmoja wa wanufaika wa msaada huo, Bw. Teophil Liundi, amemshukuru Mbunge huyo kwa kuwapatia baiskeli ambazo amesema zitawasaidia kurahisisha usafiri na kuwawezesha kufanya shughuli zao za kujipatia kipato kwa urahisi zaidi.

Amesema, baiskeli hiyo itamwezesha kufanya mizunguko ya shughuli zake kwa ufanisi zaidi na hivyo kumsaidia kufikia malengo yake ya kujiongezea kipato.