📌 Wananchi wa Busonzo wanufaika na miradi ya uhakika ya umeme, maji, elimu
📌 CCM yaahidi maendeleo Busonzo
Mgombea wa Ubunge Jimbo la Bukombe, Ndugu Doto Mashaka Biteko amewahimiza wananchi wa Kata ya Busonzo wilayani Bukombe mkoani Geita kujitokeza kwa wingi na kuwapigia kura wagombea wa CCM ili kukipatia chama hicho ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu ujao Oktoba 29, mwaka huu.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 9, 2025 wakati akiendelea na kampeni katika Kata ya Busonzo wilayani Bukombe mkoani humo.
Amesema eneo la Idoselo katika Kata ya Busonzo lilikuwa na changamoto kadhaa ikiwemo barabara na shule.
Kufuatia hali hiyo, Rais Samia alielekeza wananchi wa eneo hilo wachongewe barabara, wajengewe shule na hospitali.

“ Hapa Idoselo tumejenga Kituo Kikubwa cha Kuzalisha umeme megawati 5 ili wananchi waweze kupata umeme, tunataka kuongeza upatikanaji wa maji na baada ya uchaguzi tutapanua chanzo cha maji ili kuhakikisha kunakuwa na maji ya uhakika,” amesema Dkt. Biteko.
Ametaja vipaumbele vya CCM ni kujenga shule nyingine ya sekondari Idoselo ili kupunguza adha ya wanafunzi kwenda kusoma Busonzo.
Aidha, amewahimizi wananchi na wajumbe wa CCM kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu na kumchagua mgombea wa Urais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo pia amewaomba wananchi wamchague kwa nafasi ya Ubunge wa Bukombe pamoja na mgombea Udiwani Merikiori wa Busonzo.
Akimnadi mgombea udiwani wa Kata ya Busonzo, amesema mgombea huyo ni mchapakazi na anayetaka maendeleo hivyo, wananchi wamchague ifikapo Oktoba 29 huku akisisitiza kuwa ili CCM ishinde kwa kishindo wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura.
Naye, Mgombea wa nafasi ya Udiwani Kata ya Busonzo, John Merikiori amesema ni wajibu wa wananchi kupiga kura na kuchagua wagombea wa CCM ambao wakipata dhamana ya uongozi watahakikisha wanaleta maendeleo kwa wananchi.

