📌 Asema Dkt. Nchimbi ni mtu mwema anayejua shida za watu
📌 Mamia wajitokeza Kampeni za CCM Katoro
📌 Asema Katoro hawana mbambamba, awaomba Oktoba kuchagua wagombea wa CCM
Mgombea wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Bukombe, Ndugu Doto Mashaka Biteko amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi kimepata Mgombea Mwenza wa nafasi ya Urais, anayefaa na kujua majukumu yake ambaye ni Balozi. Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 6, 2025 wakati akiwasalimia wananchi wa Katoro kwenye Kampeni za Mgombea Mwenza wa nafasi ya hiyo ya Urais kupitia CCM, Balozi. Dkt. Nchimbi.

“ Tumepata Mgombea Mwenza anayejua kazi, anayejua shida za watu yeye ni mwalimu wa wengi nikiwemo mimi ametufundisha mengi,” amesema Dkt. Biteko
Ameendelea kubainisha sifa za Dkt. Nchimbi na kusema kuwa ni mtu mwema anayejua kumuweka karibu kila mtu na ambaye hazungumzii wapinzani katika hotuba yake ispokuwa CCM, kazi yake na kubadilisha maisha wa wananchi.
Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo, Dkt. Biteko amewaeleza wananchi wa Katoro na Geita kuwa Uchaguzi na kura yao ni maisha yao hivyo amewaomba Oktoba 29 mwaka huu wajitokeze kwa wingi kupiga kura.

Amesisitiza “ Najua Katoro hamna mbambamba, kwenu nyie hamna mechi ndogo hata mazoezi kwenu nyie mechi, nawaomba mtuchagulie madiwani na mbunge ili waungane na Dkt. Samia Suluhu Hassan ili tuweze kuleta maendeleo ya Katoro na Katoro lazima ibadilike,”
Aidha, amesema Geita inawaunga mkono Dkt. Samia na Nchimbi, wabunge na madiwani wa CCM na inahusisha Uchaguzi na maisha yao hivyo wanachagua kwa ajili ya maisha yao.


