Na Abdala Sifi – WMJJWM – Morogoro 

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema dhamira ya Serikali ni kuendelea kuwajali na kuwahudumia wazee kwa kuwa ni tunu na hazina ya Taifa.

Dkt. John ameyasema hayo Februari 24, 2025 wakati akizungumza na wazee wanaoishi katika Makazi ya Wazee Fungafunga mkoani Morogoro. 

Dkt. Jingu amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wazee katika harakati za ujenzi wa Taifa, hivyo itaendelea kuboresha huduma zinazotolewa katika makazi hayo ikiwemo huduma za afya, lishe, malazi na ustawi wa kijamii. 

“Lengo ni kuhakikisha wazee wanaishi katika mazingira salama, yenye heshima na yanayowapa faraja, kwa sababu busara na uzoefu wao ni msingi wa maadili na maendeleo ya jamii yetu. Wajibu wa Serikali na jamii kwa ujumla ni kuhakikisha wanapata huduma bora na stahiki wakati wote.” amesema Dkt. Jingu.

Aidha, amewahimiza watumishi wa makazi hayo kuendelea kufanya kazi kwa weledi, moyo wa huruma na kujituma, wakitambua kuwa wanahudumia kundi lenye heshima kubwa katika jamii.

Dkt. Jingu amekabidhi zawadi mbalimbali kwa kwa wazee hao ikiwemo vyakula na fedha kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Kwa upande wake, mmoja wa wazee wanaishi kwenye makazi hayo Daniel John, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma na mazingira ya makazi hayo. Ameeleza kwamba huduma wanazopata zinawapa utulivu wa moyo na kuwafanya wajione kuwa bado ni sehemu muhimu ya jamii.

“Tunashukuru Serikali kupitia Wizara kwa kutujali, tunapata huduma nzuri na tunaishi kwa amani, hii inatupa faraja kubwa,” amesema Mzee Daniel.

Ziara hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha makundi maalum, hususan wazee, yanapata ulinzi na huduma bora kwa mujibu wa Sera na mipango ya maendeleo.