Na Tina Makoye – WMJJWM, Dodoma
Wakuu wa Vitengo vya Habari na Mawasiliano Serikalini wa Wizara na Taasisi za Serikali wameaswa kutumia nafasi zao kueleza jamii na dunia kwa ujumla kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa programu ya kizazi chenye usawa kupitia miradi mbalimbali iliyofanywa na Wizara na Taasisi hizo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu wakati wa kikao kazi chenye lengo la kuwajengea uwezo Wakuu hao wa Vitengo kilichofanyika Februari 5, 2026, Jijini Dodoma.

Dkt. Jingu ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara yenye dhamana, imeendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara za Kisekta, Taasisi za Umma pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika utekelezaji wa Programu hiyo, kwa lengo la kuhakikisha ushirikiano wa pamoja na utekelezaji wenye ufanisi katika ngazi zote.
“Katika kutekeleza programu hii, kuna mafanikio mengi na makubwa yamepatikana nchini, mna nafasi ya kuelimisha Umma, kuibua uelewa na kuchochea ushiriki wa jamii katika jitihada za kuleta kizazi chenye usawa, hivyo kuchangia kwa kasi utekelezaji wa Sera, Sheria na Mipango mbalimbali ya Kitaifa ikiwemo Dira ya Taifa ya 2050 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2025 – 2030.amesema” Dkt. Jingu.
Aidha, Dkt. Jingu amewasihi wakuu hao wa vitengo kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kikao kwa uwazi na ushirikiano, ili kufikia matokeo yaliyokusudiwa ya kuboresha zaidi utekelezaji wa Programu, kubaini na kujadili changamoto zinazojitokeza, pamoja na kuweka mikakati na mipango endelevu itakayochangia kwa ufanisi kuimarisha usawa wa haki za kiuchumi na kijamii katika jamii zetu.

kwa niaba ya Washiriki wa kikao kazi hicho, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini kutoka Ofisi ya ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Rhoida Andusamile ameishukuru Wizara kwa kuwajengea uwezo wa kuoanisha mafanikio ya miradi yao na utekelezaji wa Program ya Kizazi Chenye Usawa na kuahidi kuendelea kutoa taarifa zao za matokeo chanya kupita vyombo mbalimbali vya Habari, mitandao ya kijamii na fursa za matukio watakayoshiriki.
Katika kuhakikisha Utekelezaji wa Ahadi za Nchi katika mkutano wa Jukwaa la kizazi chenye usawa uliyofanyika nchini Ufaransa mwezi tarehe 30 Juni – 2 Julai 2021, Tanzania inatekeleza kipengele cha Haki na Usawa wa Kiuchumi, ambayo imejikita katika maeneo manne:Uwekezaji wenye mrengo wa kijinsia katika huduma na kazi za matunzo kwenye sekta ya umma na sekta binafsi; Kazi zenye staha kwa wanawake katika sekta rasmi na sekta isiyo rasmi; Upatikanaji na umiliki wa rasilimali za uzalishaji kwa wanawake; na Kubuni na kutekeleza mipango ya uchumi mkuu inayozingatia jinsia, maboresho ya bajeti na motisha ili kupunguza idadi ya wanawake na wasichana wanaoishi katika umasikini.





