Na Sixmund Begashe, JamhuriMedia, Arusha
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imepongezwa kwa ubunifu wake katika utekelezaji wa majukumu yake yaliyosababisha mafanikio katika uhifadhi na Utalii nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, ametoa pongezi hizo leo Januari 08, 2026 Jijini Arusha wakati akipokea taarifa ya utekelezaji kazi wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA inayomaliza muda wake.

Dkt. Kijaji amesema ubunifu katika utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo, umeendana sambamba na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya uhifadhi endelevu wa urithi wa rasilimali kwa maslahi ya vizazi vijavyo na Taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa pamoja na mambo mengine, Bodi hiyo imewezesha kuongezeka kwa wawekezaji na mapato kusababisha kuimarika kwa uhifadhi, kupungua kwa uvamizi katika maeneo ya hifadhi na mapori tengefu pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia licha ya uwepo wa maeneo ya maboresho.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Naibu Katibu wa Wizara hiyo Bw. Nkoba Mabula, amemuhakikishia Waziri Kijaji kuwa Ofisi yake itaifanyia kazi taarifa hiyo iliyo kabidhiwa ili kuongeza tija zaidi katika uhifadhi na Utalii kupitia TAWA na taasisi zingine za uhifadhi nchini.

Pamoja na kuushukuru uongozi wa Wizara kwa ushirikiano mkubwa, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko amesema mafanikio mengine ni kuboresha mwitikio wa haraka katika matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kupitia doria zinazohusisha vikosi maalum vya TAWA kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori wa vijij (VGS).
Pia aliongeza kuwa katika kipindi husika TAWA iliweza kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizp kutokana na usimamizi madhubuti wa mifumo ya udhibiti wa ndani (Internal Controls) na kushirikisha jamii katika uhifadhi kupitia miradi ya jamii, uvuvi na ufugaji nyiki Kupitia Hifadhi na kutoa gawio kwa wanufaika.





