Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge amesema kuwa zaidi ya wananchi 1,000 wa Jiji la Arusha na maeneo ya jirani wamenufaika kupitia Mpango wa Tiba Mkoba wa Dkt. Samia Suluhu Hassan (Outreach Program).

Dkt. Kisenge ameyasema hayo leo jijini Arusha katika hospitali ya ALMC mkoani Arusha wakati wa zoezi la utoaji wa huduma za upimaji na uchunguzi wa afya bure zinazoendelea hospitalini hapo kwa takribani wiki moja sasa.

Kupitia kambi hiyo, wananchi wanapatiwa fursa ya kupima afya zao kwa magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo, kisukari pamoja na magonjwa mengine yanayoathiri afya ya binadamu. Huduma hizi zinalenga kusaidia wananchi kugundua matatizo ya kiafya mapema na kuchukua hatua stahiki kabla ya madhara makubwa kujitokeza.

Amesema mpango huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha huduma za kibingwa za afya, hususan magonjwa ya moyo na mengine yasiyoambukiza, zinawafikia wananchi wengi zaidi bila kujali uwezo wao wa kifedha.

“Kwa sasa, wananchi wote wenye matatizo ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza wanahimizwa kufika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre, ambayo sasa inatoa huduma hizo chini ya usimamizi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.”amesema Dkt Kisenge.

Dkt. Kisenge, amewahimiza Watanzania, hususani wakazi wa mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani, kujitokeza kwa wingi kupima afya zao mara kwa mara.

Aidha, Dkt. Kisenge ameongeza kuwa mtindo usiofaa wa maisha, hususan kutofanya mazoezi ya mwili, ni miongoni mwa sababu kubwa zinazochangia kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza nchini.

Aidha amewahimiza wananchi kuzingatia kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kula lishe bora na kupunguza matumizi ya vyakula vyenye mafuta mengi ili kujikinga na magonjwa hayo.

JKCI inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa afya bora kwa kushirikiana na taasisi za afya nchini, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi walioko mbali na makao makuu ya taasisi hiyo.