Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula wamewasili jijini Pretoria, Afrika Kusini kushiriki Mkutano wa 47 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika Machi 12 na 13, 2026 jijini humo.

Mawaziri hao, Mhe. Maghembe na Mhe. Luswetula Machi 11, 2026 wakiwa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini walipokea taarifa kutoka kwa watalaamu kuhusu majadiliano ya vikao vya utangulizi. Vikao hivyo ni Kikao cha Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi cha kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati Elekezi wa Maendeleo wa Kanda (RISDP) kilichofanyika tarehe 04 na 05 Machi 2026, Kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu kilichofanyika tarehe 07 na 08 Machi 2026 na kikao cha Kamati ya Fedha kilichofanyika Machi 09. 2026.

Waheshimiwa Mawaziri pia walipokea taarifa ya ushiriki wao katika Mkutano wa 47 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo utakaofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano uliopo majengo ya ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini.

Wakiwa kwenye ofisi hizo za Ubalozi, Waheshimiwa Mawaziri walipokea taarifa ya hali ya uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na eneo la uwakilishi iliyotolewa na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. James Bwana.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye vikao vya utangulizi.