Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia katika Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Kumbukizi ya Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere pamoja na Wiki ya Vijana Kitaifa kwa Mwaka 2025 zilizofanyika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.

Amesema kupitia falsafa hiyo, nchi imefanikiwa katika mambo mengi ikiwemo kuondoa ubaguzi, ukabila, na kujenga umoja wa kitaifa, kuimarisha utawala bora, kupinga dhuluma, dharau, chuki na kupambana na ufisadi na rushwa.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Mwenge wa uhuru ulipoasisiwa ulilenga kuidhihirishia dunia na kuonesha mfano kwa Mataifa yaliyokuwa bado chini ya udhalimu wa kikoloni, maana ya Taifa huru na uwezo wa kujitawala pasipo kuingiliwa na mtu mtu yeyote.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa Watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura, kushiriki katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea ili kusikiliza sera za vyama mbalimbali, na kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kuwachagua viongozi watakaoongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo kama ambavyo Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 zilivyobeba ujumbe wa kuhamasisha wananchi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu.

Katika kumbukizi ya Miaka 26 tangu kifo cha Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Makamu wa Rais amesema ili kuendelea kuenzi maisha na mchango mkubwa wa Baba wa Taifa, Watanzania wote ni vema kusimamia misingi mikuu aliyotuachia Mwl. Julius Nyerere.

Ametaja misingi hiyo ikiwemo kulinda uhuru wa Taifa pamoja na kudumisha umoja na amani na kusimamia haki miongoni mwa jamii, kujenga na kuimarisha maadili mema katika jamii hususan miongoni mwa vijana ambao ndiyo Taifa la sasa na la kesho.

Pia ameongeza kwamba misingi mingine ya kusimamia ni pamoja na kuwajibika kwa kila mwananchi kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha maisha na kuinua vipato na hivyo kuchangia katika ujenzi wa Taifa pamoja na uhifadhi na utunzaji wa mazingira, hususan kulinda vyanzo vya maji, upandaji wa miti na kufanya usafi wa mazingira, mambo ambayo Baba wa Taifa alikuwa mfano bora wa kuigwa.

Akihitimisha Wiki ya Vijana Kitaifa mwaka 2025, Makamu wa Rais ametoa rai kwa vijana, kuendelea kutumia ubunifu, maarifa na nguvu zao vizuri zaidi na Serikali inawaamini na itawaunga mkono. Amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwenye elimu, ujuzi, teknolojia, ubunifu, michezo na utamaduni ili kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza.

Aidha, Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2025 – 2030) imeweka lengo la kuanzisha vituo vya uwezeshaji vijana kiuchumi katika mikoa, pamoja na kuzalisha ajira kwa vijana zipatazo milioni 8.5 ifikapo 2030.


Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuyatenda maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo, kwa kuimarisha uchumi wa Taifa, kukuza heshima ya Tanzania kimataifa, na kulinda amani na umoja wa Watanzania.


Ameongeza kuwa ni jukumu la kila mtanzania kuenzi urithi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa uadilifu, uwajibikaji na uongozi wa kujituma kwa ajili ya watu, kuendeleza mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi.

Awali akisoma risala ya kuhitimisha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025, Kiongozi wa mbio hizo Ismail Ali Ussi amesema wananchi wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mitambo ya kuchimbia visima ambayo imesaidia katika upatikanaji wa huduma za maji safi na salama.

Pia amesema wananchi wamemshukuru Rais kwa ongezeko la mshahara ambalo limeboresha ustawi wa wafanyakazi na kuongeza ari ya ufanyaji kazi kwa watumishi wa umma nchini iliyopelekea wananchi kupata huduma bora.

Amesema Mwenge wa Uhuru 2025 umekagua miradi ya vijana walionufanika na mikopo ya asilimia kumi ambapo wameshukuru kwa kurejesha mikopo hiyo ambayo imesaidia kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara. Aidha amesema Vijana wamemshukuru Rais kwa kuanzisha shule za amali hapa nchini na kujenga uendelezaji Vyuo vya Veta nchini.

Amesema uanzishaji wa Vyuo na Shule utasaidia vijana kupata ujuzi mbalimbali na kujiajiri kupitia juzi mbalimbali ikiwemo kutumia sayansi na teknolojia katika kutafuta utengenezaji wa bidhaa na kutafuta masoko ya bidhaa na malighafi.

Katika Maadhimisho hayo, Kitabu cha Miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kimezinduliwa ambapo kimelenga kuhifadhi kumbukumbu muhimu za Kihistoria, hususan chimbuko, maendeleo na mchango wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika kujenga mshikamano wa kitaifa, uzalendo na kuhamasisha maendeleo. Kitabu hicho pia kinaelezea umuhimu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kama alama ya mshikamano wa Watanzania wote bila kujali tofauti za dini, kabila au itikadi.