Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewakaribisha wawekezaji kutoka Ghana kuwekeza nchini kupitia fursa nyingi zilizopo katika sekta ya madini, kilimo, utalii, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), elimu na huduma za jamii.

Dk Mpango ameeleza hayo alipozungumza na Balozi wa Ghana nchini anayemaliza muda wake, Damptey Bediako Asare, Ikulu Dar es Salaam.

Dk Mpango amesema ni muhimu kuendelea kushirikiana zaidi katika uwekezaji na biashara kupitia Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCTFA)

Alisema Tanzania na Ghana zimeendelea kunufaika na uhusiano uliopo wa kihistoria ulioanza tangu kipindi cha utafutaji uhuru wa mataifa hayo ukichagizwa na urafiki wa baba wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Nyerere na Kwame Nkrumah.

Amesema Tanzania inatambua mchango wa Ghana katika ukombozi wa mataifa ya Kusini mwa Afrika wakati wa kupigania uhuru.

Alisema mataifa hayo mawili yameendeleza ushirikiano uliopo, kwa sasa yamejikita zaidi katika uhusiano wa kiuchumi akisisitiza ushirikiano zaidi unahitajika katika eneo hilo.

Kadhalika, Dk Mpango aliipongeza Ghana kwa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa yaliyofanyika Dar es Salaam mwaka 2024.

“Kupitia maonesho hayo, ushirikiano wa kiuchumi baina ya mataifa haya mawili umeongezeka na kutoa ujumbe kwa mataifa mengine umuhimu wa kutoa kipaumbele katika kushirikiana na mataifa ya Kiafrika yenyewe,” amesema.

Kwa upande wa Balozi Asare ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano aliopata kipindi chote alichohudumu nchini.

Amesema amewasilisha salamu za Rais wa Ghana, John Mahama ambazo amezitoa kwa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali kwa kuendeleza ushirikiano na kuiunga mkono Ghana katika nyanja mbalimbali hususani katika majukwaa ya kimataifa.

Katika hatua nyingine, Dk Mpango alitoa salamu za pole kwa serikali na wananchi wa Ghana kutokana na ajali ya ndege iliyotokea hivi karibuni na kusabibisha vifo vya watu wanane akiwemo Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Mazingira wa nchi hiyo.