Na Mwandishi Maalum

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameikaribisha Vietnam kuchangamkia fursa za uwekezaji nchini kama vile kilimo, viwanda vya nguo na viwanda vingine vya uzalishaji.

Dk Mpango amesema hayo alipokutana na kuzungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Ho Duc Phoc kando ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (FfD4) unaofanyika jijini Sevilla, Hispania.

Alisema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na inatatua changamoto zinazojitokeza katika uwekezaji kupitia majukwaa ya utoaji maoni.

Dk Mpango alisema serikali ipo tayari kushirikiana na Kampuni ya Vietnam ya Viettel inayomiliki mtandao wa Simu wa Halotel kuendelea kufikisha huduma bora ya mtandao, ikiwemo ya 5G.

Aliishukuru Serikali ya Vietnam kwa kuridhia soko la bidhaa za Tanzania zikiwemo korosho na bidhaa za misitu.

Alisema ni muhimu kukuza ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Vietnam katika uwekezaji, kilimo, biashara, masuala ya ulinzi na kushirikiana pia katika masuala ya kikanda na kimataifa.

Dk Mpango alisema Serikali ya Tanzania inathamini ushirikiano baina yake na Vietnam ambao umedumu kwa miaka 60 sasa.

Alisema Vietnam ni kati ya nchi za kwanza zilizofungua ubalozi baada ya uhuru na kushirikiana na Tanzania kupitia serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi.

Dk Mpango alisema Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano uliopo na Vietnam ikiwa ni pamoja na kuungana mkono kwenye masuala yenye maslahi ya pamoja katika majukwaa ya kimataifa.

Aliipongeza Vietnam kwa kuandaa Tume ya Kwanza ya Ushirikiano ya Pamoja (JPC) mwaka 2014.

Alisema Tanzania itaandaa Tume ya Pili ya Pamoja ya Ushirikiano baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Phoc alisema ushirikiano wa kiuchumi unaendelea kuimarika na kwamba Tanzania inatumia soko la Vietnam
kuuza korosho na bidhaa za misitu na kila mwaka mauzo ya biashara hizo hufikia Dola milioni 150.

Alisema uchumi wa mataifa hayo mawili unaendelea kutegemeana kwa kuwa Vietnam inazalisha bidhaa ambazo zinauzwa Tanzania yakiwemo mavazi na vyakula.

Phoc alisema ni vema kuendelea kuimarisha ushirikiano zaidi kwa kuwa bado yapo maeneo yanayoweza kuwekezwa zaidi kupitia mashirika mbalimbali ya kibiashara na uwekezaji.

Aliishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Vietnam katika majukwaa ya kimataifa na hivyo kudumisha ushirikiano mzuri uliopo.

Wakati huohuo, Dk Mpango alikutana na kuzungumza na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Maendeleo wa Denmark, Elsebeth Søndergaard Krone.

Aliishukuru Denmark kwa mchango iliotoa katika maendeleo ya Tanzania katika sekta za uchumi ambazo zimebadili maisha ya Watanzania ikiwemo miundombinu, fedha, afya na maji.

Dk Mpango alishiriki mkutano wa pembezoni wa nchi zinazoendelea ulioongozwa na Waziri Mkuu wa Nepal, Kadga Sharma Oil na kuhudhuriwa na mataifa rafiki yaliyoendelea.

Mkutano huo ulijadili tathmini ya utekelezaji wa azimio la Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea uliofanyika Doha, Qatar mwaka 2023.