Na Mwandishi Maalum, New York

Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango, ametoa mwito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji binafsi, akisisitiza kuwa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ni nguzo muhimu ya kufungua fursa kubwa za kiuchumi za Tanzania.

Akizungumza katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani, lililofanyika New York, pembeni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA), Dkt Mpango alisema, PPP siyo tu njia ya kuchangisha dola bilioni 185 ambazo Tanzania inahitaji ndani ya miaka mitano ijayo, bali pia ni njia bora ya kuhakikisha ustawi wa pamoja kati ya Watanzania na wafanyabiashara wa Marekani.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati akifungua Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani lililofanyika kando ya Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 80) Jijini New York nchini Marekani. Tarehe 22 Septemba 2025.

“Sekta binafsi ni mshirika muhimu katika jitihada zetu za maendeleo,” alisema, akibainisha kuwa Tanzania imefanya mageuzi katika mfumo wa uwekezaji ili kuunda mazingira rafiki zaidi kwa PPP, kuanzia sekta ya nishati na usafirishaji hadi afya na teknolojia ya kidijitali,” Dkt Mpando alisema.

Makamu wa Rais alitaja mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) yenye urefu wa kilomita 2,561, inayofadhiliwa kwa kiasi kikubwa kupitia PPP, kuwa chachu ya kuunganisha Tanzania na masoko ya kikanda yenye zaidi ya walaji milioni 300.

“Kiwanda kilichopo Tanzania kinaweza kuhudumia kwa urahisi Afrika Mashariki na Kati,” alisema, akiongeza kuwa Maeneo Maalum ya Uwekezaji (SEZs) yanayounganishwa na bandari na kuendeshwa kwa nishati jadidifu yako tayari kwa uwekezaji wa pamoja.

Tanzania, ikiwa na akiba kubwa ya grafiti, nikeli na lithiamu, inatafuta ushirikiano na Marekani siyo tu katika uchimbaji, bali pia katika uongezaji thamani kupitia PPP kwenye uchakataji, uzalishaji betri na uendelezaji wa viwanda vya nishati safi.

Kuenea kwa intaneti na matumizi makubwa ya fedha kwa simu kumefanya Tanzania kuwa kitovu kinachochipukia cha huduma za kifedha na kidijitali. PPP na makampuni kama Visa ambayo tayari yanaendesha kituo cha ubunifu Dar es Salaam yanaweza kusaidia kupanua ekosistemu za ubunifu.

Kwa kuwa ni asilimia 24 tu ya ardhi yake inayofaa kwa kilimo ndiyo inayolimwa, Tanzania inakaribisha PPP katika kilimo sahihi, teknolojia za droni, kilimo kinachoendeshwa na akili bandia (AI), na uongezaji thamani mazao ili kukidhi mahitaji ya chakula ya Afrika na dunia” alisema.

Dk Mpango alizishauri kampuni za Marekani zinazozalisha dawa na vifaa vya tiba kuanzisha viwanda vya ndani kupitia PPP, hatua itakayopunguza utegemezi wa Afrika kwa dawa zinazoagizwa kutoka nje.

Dkt Mpango alieleza kuwa serikali inaendelea kufanya mageuzi ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu bora cha PPP. Usajili wa biashara sasa huchukua masaa 24 badala ya siku 14, huku vibali vya uwekezaji vikitoolewa ndani ya masaa machache kupitia kituo cha huduma kwa pamoja. Aidha, serikali inawekeza kwenye elimu na ujuzi ili kuhakikisha miradi ya PPP inapata rasilimali watu yenye uwezo.

“Tanzania imeendelea kuwa na utulivu wa kisiasa kwa miaka 60. Miundombinu yetu inabadilika kwa kasi, na makampuni yaliyopo tayari nchini yamekuwa yakipata faida kati ya asilimia 20–30. Huu ndio wakati sahihi kwa wafanyabiashara wa Marekani kuingia kupitia ubia ulio na mpangilio,” alisema Dkt. Mpango.

Kwa kuzingatia kuwa Mpango wa Ukuaji wa Biashara kwa Afrika (AGOA) unatarajia kuisha muda wake ndani ya siku chache, Dkt. Mpango alisema kuhuishwa kwake kutakuwa na manufaa kwa Marekani na Afrika kwa ujumla. Aliwahimiza wawekezaji wa Marekani kuchukua hatua haraka, akibainisha kuwa “wengine bado wanachambua, huku washindani kutoka kanda nyingine tayari wakichukua hatua.” alisema.