Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,
Dar es Salaam
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa jengo jipya la wageni maarufu (VVIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) – Terminal 3.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 15, 2025 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila RC wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema uzinduzi wa jengo hilo utafanyika Januari 16, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) – Terminal 3 Jijini Dar es Salaam.

Sambamba na hayo amebainisha kuwa ujenzi wa jengo ni kwa lengo la kuboresha huduma za mapokezi kwa wageni waalikwa, watu mashuhuri pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali wanaoingia nchini.
Amesema jengo hilo limejengwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa, mbapo kiongozi yeyote atakayeingia humo atapata huduma zote za kijamii hatua ambayo imekusudiwa kuongeza ubora wa huduma katika sekta ya usafiri wa anga na kuinua hadhi ya Taifa la Tanzania kimataifa.
“Mradi huu ni maalum kwa ajili ya kuwahudumia wageni wakubwa, wakiwemo viongozi wa kitaifa na kimataifa pamoja na watu mashuhuri kutoka sehemu mbalimbali duniani,” amesema Mhe. Kunenge.

Ameongeza kuwa ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuboresha taswira ya Jiji la Dar es Salaam kama lango kuu la kuwakaribisha wageni wa ndani na nje ya nchi, sambamba na kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga.
Uzinduzi wa jengo la VVIP katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere unatarajiwa kuongeza viwango vya huduma, kuboresha uzoefu wa wageni na kuinua zaidi hadhi ya Tanzania katika masuala ya usafiri wa anga kikanda na kimataifa.



