Uzinduzi wa kampeni Jimbo la Songea mjini.

Na Cresensia Kapinga, Jamuhuri ,Songea.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Afya na maswala ya Ukimwi ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Elibariki Kingu amemuombea kura mgombea wa nafasi ya Rais kupitia chama Cha Mapinduzi (CCM)Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza Dk. Emmanuel Nchimbi, Dk. Damas Ndumbaro mgombea wa nafasi ya ubunge Jimbo la Songea mjini na wagombea wa wanafasi ya udiwani kupitia chama hicho na kwamba wananchi waone umuhimu wa kuwapigia kura za ndio Oktoba 29.

Akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika katika viwanja vya michezo vya Kiblang’oma Kata ya Lizaboni Jimbo la Songea mjini ambapo Kingu alikuwa mgeni rasmi alitumia nafasi hiyo kunadi Ilani ya chama Cha Mapinduzi ( CCM) 2025/ 2030.

Alisema katika kipindi cha miaka 5 iliyopita kwa Halmashauri ya Manispaa ia Songea imeweza kujenga vituo vya Afya 8 pamoja na hospitali ya rufaa inayojengwa katika kata ya Mwengemshindo ,wamejenga shule tatu maalumu pamoja na vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari, wameboresha miundombinu ya Barabara kwa kiwango cha Rami, wamejenga vivuko na madaraja, Umeme katika kata zote, mradi wa maji mkubwa wa miji 28 ambao umetumia zaidi ya sh. Bilioni 147.

Alieleza zaidi kuwa Dk.Samia amewawezesha wakulima kupata pembejeo za kilimo za ruzuku na hivi sasa kuna Ujenzi wa chuo kikuu cha taaluma ya uhasibu unaendelea kujengwa katika eneo la Mlete jambo ambalo limeonesha kuwa Dk. Samia na Dk.Ndumbaro wanapaswa kupewa mitano tena ili waweze kukamilisha miradi aliyoianzisha na wananchi wa Jimbo la Songea waweze kunufaika.

Katika uzinduzi huo wagombea wa nafasi ya udiwani kutoka kata 21 pamoja na madiwani wateule wa viti maalum walisimama kujinadi wao wenyewe pamoja na kuwaombea kura Rais Dk Samia Suluhu Hassan , mgombea mwenza Dk. Emmanuel Nchimbi pamoja na Dk. Ndumbaro ili waweze kutekeleza Ilani ya chama cha Mapinduzi.

Kwa upande wake mgombea wa nafasi ya Ubunge Dk. Ndumbaro amewashukuru wananchi wa Jimbo hilo kwa kujitokeza kwa wingi na kwamba kazi aliyonayo mbele ni utekelezaji wa Ilani ambayo amekabidhiwa kwenye mkutano huo na mwenyekiti wa CCM Wilaya Mwinyi Msolomi na amewaahidi hatowaangusha.