Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media, Dar es Salaam
Novemba 10, 2025 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa wabunge sita katika nafasi 10 anazopewa kikatiba. Walioteuliwa ni Dk. Rhimo Nyansaho, Balozi Dk. Bashiru Ally Kakurwa, Dk. Dorothy O. Gwajima, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo, Adullah A. Mwinyi na Balozi Khamis Mussa Omar.
Uteuzi huu umeniburudisha. Katika nyakati ambapo nchi inahitaji viongozi wabunifu, wachapakazi na wenye maono, jina la Dk. Nyansaho limeendelea kung’ara. Ni kiongozi ambaye ameonyesha uwezo wa kusimamia taasisi mbalimbali zenye umuhimu mkubwa katika uchumi na maendeleo ya taifa. Rais Samia kumteua kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania si imenifurahisha, bali imethibitisha kuwa kujituma na uadilifu inalipa.

Kwa sasa, Dkt. Nyansaho anashikilia nafasi kadhaa muhimu zinazodhihirisha wigo na uwezo wake wa kiuongozi. Ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) aliyeteuliwa Mei 26, 2025, ambako amesimamia mageuzi makubwa katika utendaji na uwajibikaji wa taasisi hiyo kwa muda mfupi aliokaa.
Amehakikisha mafao ya wanachama yanatolewa kwa wakati, masilahi ya wafanyakazi yanaboreshwa, huku akihimiza uboreshaji wa huduma kwa njia za kidijitali. Huu ni ushahidi wa uongozi wa kisasa unaotumia teknolojia na weledi kusogeza huduma karibu na wananchi.
Mbali na PSSSF, Nyasaho ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO). Dk. Nyansaho amekuwa sehemu ya mapinduzi ya sekta ya umeme nchini. Chini ya uongozi wake, TANESCO imeendelea kuimarisha miradi mikubwa ya kuzalisha na kusambaza umeme ikiwemo Bwawa la Julius Nyerere, miradi ya umeme wa upepo na jua, na upanuzi wa gridi ya taifa.

Uongozi wake umejikita katika kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha nishati ya umeme Afrika Mashariki. Ni katika uongozi wake wa Bodi, Tanzania imefikisha megawati 4,031 na kuzipita nchi zote za Afrika Mashariiki.
Katika sekta ya makazi, Dk. Nyansaho ni Mwenyekiti wa Bodi ya Watumishi Housing Investment (HIC), taasisi inayowezesha upatikanaji wa nyumba bora kwa watumishi wa umma. Kupitia HIC. Amesisitiza ujenzi wa nyumba zenye ubora na bei nafuu, sambamba na kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika ujenzi wa nyumba za makazi.
Hajaishia hapo, Dk. Nyansaho ni Mjumbe wa Bodi ya TANAPA, Mjumbe wa Bodi ya TIC, Mjumbe wa Bodi ya Benki ya Azania, na Mjumbe wa Bodi ya Management and Development for Health (MDH). Majukumu haya yanamuweka katika nafasi ya kipekee ya kuchangia sera, uwekezaji, hifadhi ya mazingira, afya ya jamii, na maendeleo ya kifedha — maeneo yote muhimu kwa ustawi wa taifa.
Kabla ya wadhifa wa sasa, aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Azania, nafasi iliyompa uzoefu mkubwa katika masuala ya kifedha, biashara na uongozi wa kimkakati. Uzoefu huo umechangia kumjenga kuwa kiongozi anayejua kuunganisha taaluma na matokeo halisi.

Kwa kuangalia majukumu haya yote, ni wazi Dk. Nyansaho ni kiongozi mwenye maono mapana, anayefanya kazi kwa ufanisi na kuacha alama katika kila taasisi anayosimamia. Uteuzi wake katika Bunge ni ishara ya imani kubwa ya Rais Samia Suluhu Hassan katika uwezo wake wa kuchangia mijadala ya maendeleo ya taifa kwa ufanisi na maarifa.
Kwa hakika, Tanzania inajivunia kuwa na kiongozi mwenye maono, uthubutu na weledi kama Dk. Rhimo Nyansaho — kiongozi anayechanganya uzoefu wa sekta binafsi na umma, na ambaye anaendelea kuwa dira ya uongozi wa kizazi kipya. Hongera Dk. Nyasaho kwa uteuzi huu.




