
Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ali, amesema kuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anastahili kupigiwa kura za ndiyo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika kesho Oktoba 29, 2025, kutokana na sifa na uongozi wake bora.
Akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni za CCM uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Dkt. Bashiru amesema kuwa Dkt. Samia ni kiongozi anayejali watu na mahitaji yao, hasa katika sekta ya afya ambapo amewezesha huduma bora na kupunguza vifo vya watoto na akina mama wajawazito. Aidha, amebainisha kuwa Dkt. Samia ni kiongozi mchapakazi na mbunifu ambaye amethibitisha uwezo mkubwa wa uongozi katika kuandaa na kusimamia kampeni za chama kwa miezi miwili bila kuchoka.
Amesema kuwa katika kipindi cha kampeni, Dkt. Samia ameonyesha moyo wa kujituma na kujitolea, hali iliyowafanya wagombea wengine wa CCM kuiga mfano wake wa uchapakazi. Aidha, ameeleza kuwa wakati wa janga la Uviko-19, Dkt. Samia alionyesha ubunifu wa kipekee kwa kuelekeza fedha za mkopo wa kimataifa katika miradi ya maji, elimu, afya na barabara, hatua iliyosaidia kuboresha huduma za kijamii nchini.
Dkt. Bashiru amebainisha kuwa Dkt. Samia ni kiongozi mtulivu na mstahimilivu ambaye amesimamia kampeni za uchaguzi kwa amani bila kujibu mashambulizi ya maneno binafsi dhidi yake, familia yake na chama chake. Amesema kuwa utulivu huo umechangia kulifanya taifa kuendelea kuwa na amani na umoja wakati wa uchaguzi.

Amesisitiza kuwa Dkt. Samia ni jasiri na mwenye msimamo thabiti katika kulinda maslahi ya nchi, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, pamoja na usalama wa taifa. Aidha, amesema kuwa chini ya uongozi wake, mifumo ya ukusanyaji kodi na usimamizi wa rasilimali za umma imeimarishwa, hatua iliyopunguza mianya ya uvujaji wa mapato ya serikali.
Pia, Dkt. Bashiru amesema kuwa Dkt. Samia ni kiongozi mcheshi na mchangamfu ambaye anapenda kuona Watanzania wakifurahia maisha baada ya kazi, hasa kupitia sekta za michezo, sanaa na utamaduni ambazo zimepata maendeleo makubwa chini ya uongozi wake.
Pia, amesema kuwa kwa sifa hizo zote za uongozi, ubunifu, uthubutu na utu, Watanzania wana kila sababu ya kumpigia kura za ndiyo Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi wa kesho ili aendelee kuiongoza nchi kwa amani, umoja na maendeleo.



