MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki sala fupi na kuweka shada la maua katika kaburi la Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa.

Dkt. Samia kabla ya kushirki sala na kuweka shada la maua katika kaburi hilo, aliwasha mshumaa.

Ameshiriki matukio hayo leo Jumatano Septemba 24, 2025 katika kaburi la Hayati Mkapa kijijini kwao Lupaso Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara.

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akiomba dua kwenye Kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa, Lupaso, Masasi mkoani Mtwara tarehe 24 Septemba, 2025.

Alipowasili hapo, Dkt. Samia alienda moja kwa moja kwenye kaburi, akawasha mshumaa kisha ikafuata sala fupi na kuweka shada la maua.

Sala fupi iliongozwa na Padri Cyril Massawe ambaye ni Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Teresia wa Mtoto wa Yesu Lupaso.

Katika sala hiyo, Dkt. Samia na ujumbe wake walimuombea Hayati Mkapa aliyefariki dunia Julai 23, 2020.

Padri Massawe pia alimuombea Dkt. Samia ili Mwenyezi Mungu azidi kumlinda katika kuiongoza nchi na wakati huu wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Dkt. Samia alipowasili alipokelewa na wana familia ya Hayati Mkapa akiwamo Nicholas Mkapa na Wiliam Erio pamoja na Chifu Nkonona Mkapa V.

Dkt. Samia yuko katika kampeni za Uchaguzi Mkuu katika Mkoa wa Mtwara.