MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameacha alama kubwa za kihistoria mkoani Simiyu anapohitimisha ziara yake leo, kabla ya kuelekea Mwanza kuandika historia nyingine kwa kufungua rasmi daraja la sita kwa urefu barani Afrika, la JP Magufuli, Kigongo – Busisi.

Mhe. Rais Samia leo Alhamis, tarehe 19 Juni 2025, anamaliza ziara yake ya siku tano mkoani Simiyu kwa kuweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa maji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ulioko Nyashimo, Busega, utakaotoa maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya kupunguza au kumaliza changamoto ya huduma hiyo katika maeneo mbalimbali ya wilaya za mkoa huo.

Ziara ya Mhe. Dkt. Samia katika wilaya zote za Mkoa wa Simiyu, imeacha alama na kumbukumbu kubwa za kihistoria katika maeneo mbalimbali, hususan katika sekta ya mifugo, kilimo, maji na jinsi ambavyo mikutano yake imevutia maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza, kila alikozungumza na wananchi kwenye miradi au mikutano ya hadhara, tangu siku ya kwanza alipopokelewa mkoani humo, eneo la Nyamikoma, Wilaya ya Busega, Jumapili tarehe 15 Juni 2025.

Katika eneo la mifugo, Dkt. Samia alizindua kampeni ya kitaifa ya mpango wa miaka mitano ya chanjo na utambuzi wa mifugo nchi nzima. Kinachofanya kampeni hiyo iwe ya kihistoria ni ukweli kuwa mara ya kwanza na mwisho Tanzania ilifanya chanjo hiyo wakati wa serikali ya awamu ya kwanza, chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Jambo la pili la kihistoria katika kampeni hiyo ya chanjo na utambuzi wa wanyama ni faida kubwa zitakazoletwa na hatua hiyo muhimu, ambapo itasaidia kulinda afya ya mifugo (na wafugaji wenyewe), kuongeza uzalishaji na ubora, na kusaidia mazao ya mifugo ya Tanzania kupata uhakika wa soko la ndani na nje ya nchi, ikizingatiwa kuwa nchi yetu ni mojawapo ya nchi zenye mifugo wengi barani Afrika.

Kwa umuhimu wa hatua hiyo, Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT), kupitia kwa mwenyekiti wake, Ndugu Murida Mshota Marocha, walimkabidhi Mhe. Rais Samia tuzo ya heshima na shukrani, wakitambua itaimarisha na kuiinua zaidi sekta ya mifugo, ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania, kwa kuchangia asilimia 6.2 ya pato la taifa na kuwa chanzo cha ajira na kaya milioni 4.6 nchini.

Eneo jingine ambalo Mhe. Rais Samia ameacha alama ya kukumbukwa ni maelekezo yake mahsusi yanayolenga kulinda na kuinua kilimo cha mazao ya kibiashara mkoani humo, hususan zao la kihistoria linalobeba uchumi wa wa wananchi wa Simiyu, pamba na zao lingine ambalo limeanza kulimwa kwa kasi, la mbaazi.

Mbali ya maelekezo kwa Wizara ya Kilimo kuhusu utoaji wa ruzuku ya mbolea, mbegu na viuatilifu, ufuatiliaji wa hali ya soko na bei nzuri, usimamizi wa ushirika, mifumo ya umwagiliaji, upatikanaji wa zana za kilimo, kuwahakikishia sera rafiki wawekezaji wa viwanda vya kuchakata pamba, pia Mhe. Rais Samia alielekeza wizara zingine za kisekta, kushirikiana na Serikali mkoani Simiyu, kuhakikisha mazao ya pamba na mbaazi yanapanda hadhi, ambapo mathalani mnada wa kwanza wa mbaazi utafanyika Ijumaa, Bariadi.

Uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa maji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wilayani Busega, kutoka Ziwa Victoria yatakayosambazwa kuhudumia wananchi maeneo mbalimbali ya wilaya, nayo ni historia nyingine mkoani Simiyu, kutokana na ukweli kuwa ni mradi mkubwa, utakaokuwa suluhisho la changamoto ya baadhi ya maeneo ya mkoa huo kupata maji safi, salama na bora.

Kabla ya uwekaji wa jiwe hilo la msingi, mapema leo, Mhe. Rais Samia atafungua mradi wa maji katika mji wa Lamadi, na kuzungumza na wananchi wa Busega, kisha kuelekea Mwanza ambako atafanya uzinduzi rasmi wa Daraja la JP Magufuli, Kigongo – Busisi, ambalo ni daraja la sita kwa urefu Afrika, lililojengwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania.

Rais Samia alifanya majumuisho rasmi ya ziara yake jana Jumatano, tarehe 18 Juni 2025, katika mkutano mkubwa wa hadhara Bariadi, akitokea Maswa ambako pia alizungumza na umati wa maelfu ya watu, kama ilivyokuwa maeneo mengine ya Nyakabindi, Mwanhuzi – Meatu, Itilima na Maswa, ambako alifika na kuzungumza na wananchi katika maeneo ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo mkoani humo au mikutano wa hadhara.