Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa Agosti 9, 2025 kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Urais kwa tiketi ya CCM katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, ametoa taarifa hiyo leo Agosti 8, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato wa uchukuaji wa fomu za wagombea.

Amesema Dkt. Samia ataambatana na mgombea mwenza wake, John Nchimbi, kwenda kuchukua fomu katika ofisi za Tume Njedengwa saa 4:50 asubuhi. “Jana Agosti 7, 2025, Tume ilitoa ratiba ya uchukuaji fomu kuanzia Agosti 14 hadi 27 kwa wagombea mbalimbali, huku kwa wabunge ikianza Agosti 14,” alisema Makalla.

Makalla ameeleza kuwa baada ya kupokea ratiba hiyo, maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu yamepamba moto, huku mchakato wa kupata mgombea wa Urais na Mgombea Mwenza kwa upande wa Zanzibar ukiwa umeshakamilika.

Aidha, amesema baada ya kuchukua fomu, Dkt. Samia atapokelewa katika Ofisi za CCM Makao Makuu Dodoma na kisha kusalimiana na wananchi.

Ikumbukwe kuwa Dkt. Samia atachukua fomu ya kugombea Urais kwa kipindi cha pili cha miaka mitano, ili kukamilisha awamu yake ya pili ya uongozi.