Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo anatarajiwa kufanya mkutano mkubwa wa kampeni mjini Bukoba, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani Kagera ambayo imepata mwitikio mkubwa wa wananchi.
Jana, Dkt. Samia alifanya mikutano ya hadhara katika maeneo ya Muleba, Kyaka na Karagwe, ambapo aliwaeleza wananchi juu ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, hususan katika sekta za elimu, afya, barabara, maji na nishati.
Akiwa Muleba na Kyaka, Dkt. Samia aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kasi zaidi, huku akibainisha kuwa lengo kuu ni kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia Watanzania wote bila ubaguzi.
“Tumefanya mengi katika miaka hii mitano, lakini bado safari ya maendeleo inaendelea. Tunataka kuona kila kijiji kinapata maji safi, umeme, huduma za afya, kila mtoto anasoma katika mazingira bora na kila mwananchi ananufaika na uchumi wa nchi yake,” alisema Dkt. Samia jana katika moja ya mikutano yake.
Aidha, aliwataka wananchi wa Kagera kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa huo ndiyo msingi wa maendeleo na utulivu wa taifa. Alisema amani ndiyo urithi mkubwa unaowezesha serikali kutekeleza miradi mikubwa na kuvutia uwekezaji.
Leo, mgombea huyo wa CCM anatarajiwa kuhitimisha kampeni zake mkoani Kagera kwa mkutano mkubwa wa hadhara utakaofanyika Bukoba Mjini, ambapo atazungumza na wananchi kuhusu Ilani ya uchaguzi na mipango ya maendeleo ya miaka mitano ijayo chini ya serikali ya CCM.
