Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali yake imefanikiwa kufanya mageuzi makubwa ya kisheria na kimfumo yaliyolenga kujenga mazingira bora ya biashara na kurejesha imani ya sekta binafsi kuwekeza nchini.

‎Dkt. Samia ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Oktoba 28, 2025, jijini Mwanza, wakati wa kufunga kampeni za CCM katika Uwanja wa CCM Kirumba, kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika kesho Jumatano, Oktoba 29, 2025.

‎Akimshukuru Mwenyezi Mungu na Watanzania kwa ushirikiano waliompa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Dkt. Samia amesema serikali ya awamu ya sita imeendeleza miradi mikubwa iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, huku ikizindua miradi mipya ya kimkakati inayochochea uchumi.

‎Aidha, amebainisha kuwa usimamizi mzuri wa sekta ya fedha na uboreshaji wa mifumo ya makusanyo ya kodi umewezesha serikali kuimarisha uchumi wa taifa, kuongeza uwezo wa kifedha wa serikali, na kuboresha maslahi ya watumishi wa umma.

‎Ameongeza kuwa serikali pia imeimarisha taasisi za utoaji haki, ikiwemo kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, hatua ambayo imeongeza uaminifu katika mifumo ya haki nchini.          

.