Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wakazi wa Mkoa wa Tanga kukaa ‘mkao wa kula’ kutokana na mipango ya miradi ya maendeleo itakayoufungua mkoa huo.
Amesema akipewa tena ridhaa ya kuiongoza serikali ijayo ya Tanzania, atairejesha Tanga ya viwanda kwani viwanda ni moja ya kipaumbele cha serikali katika miaka mitano ijayo.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 29, 2025 kwenye Viwanja
vya Usagara jijini Tanga alipohutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni.

“Wana Tanga mkae mkao wa kula. Tunataka kuirejesha ile Tanga ya viwanda,” alisema.
Amesema tayari Tanga imekuwa na mafanikio na maendeleo makubwa
kutokana na maboresho ya Bandari ya Tanga ambayo itakuwa na bohari ya mafuta na gesi.
Kutokana na maboresho hayo, bandari hiyo itaongeza ajira 2,100 kwa wana
Tanga na kunyanyua uchumi wa wananchi wake.
Aidha, amesema Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP)
umefikia asilimia 84 na umetoa ajira 1,300 kwa wakazi wa Chongoleani na jumla
ya ajira 2,000 ndani ya Tanga.
Akizungumza mambo mazuri yajayo kwa wana Tanga, Dkt. Samia amesema Serikali itajenga reli ya Tanga – Arusha – Musoma ya kilometa 1,108 ambayo itaongeza fursa za ajira na kukuza uchumi.

Amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana
na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) watajenga Barabara ya Handeni- Singida.
Ameutaja mkakati mwingine kuwa ni kuipanua Barabara ya Dar es Salaam –
Chalinze – Segera kwa nia ya kupunguza msongamano wakati Mkoa wa Tanga
ukifunguka kiuchumi.
Katika kuirejesha Tanga ya viwanda, Dkt. Samia amesema kutajengwa Kiwanda
cha Chai Korogwe, huku Kiwanda cha Foma kikiwa kimeshafufuliwa,na Kiwanda
cha Saruji Tanga kimepanuliwa na kuongeza uzalishaji na kunajengwa kiwanda
cha kuunganisha magari ya kubeba wagonjwa(ambulance).
“Haya yote yanaongeza uwekezaji, hivyo maeneo yaliyokamatwa na watu
ambayo hayajaendelezwa yatwaliwe na kupewa wawekezaji,” amesema Dkt.
Samia.

Amebainisha kuwa kutajengwa viwanda viwili vya sukari, kimoja katika Bonde la
Pangani kwa sukari ya majumbani na kingine Tanga kwa sukari ya viwandani.
Pia katika bonde hilo kutakuwa na skimu ya umwagiliaji itakayotoa ajira 20,000
itakayojengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 87.
Amewaahidi machinga kuwa serikali yake ijayo itawajengea soko lenye uwezo
wa kuwahudumia wafanyabiashara 1,400 kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.9,
pamoja na ujenzi wa kiwanda cha dawa na vifaa tiba.
Akiwa Pangani, ameahidi kukamilisha Daraja la Pangani na Barabara ya Tanga –
Pangani – Makurunge, pamoja na ujenzi wa soko la kimataifa la samaki Kipumbwi.
Akiwa Muheza, mbali ya kuahidi kujenga na kukamilisha barabara za Muheza –
Pangani kilometa 45 na Muheza – Amani kilometa 40,mgombea huyo wa Urais
wa CCM ameahidi serikali ijayo itajenga kongani za viwanda vya matunda na
viungo.

.