Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi Serikali yake itakayoundwa endapo atachaguliwa kuingia madarakani mwakani, itatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa kingo za kudumu katika Mto Kanoni, hatua itakayomaliza tatizo la mafuriko linaloikumba Bukoba Mjini kwa miaka mingi.
Akizungumza Oktoba 16, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Viwanja vya Kaitaba, Dkt. Samia amesema Serikali tayari imekamilisha taratibu zote muhimu za maandalizi ya mradi huo ambao utaanza kutekelezwa muda wowote kuanzia sasa.
“Ninafahamu ndugu zangu kuhusu changamoto ya mafuriko ya mara kwa mara katika Mto Kanoni,” alisema Dkt. Samia. “Niwajulishe kwamba tayari tumeanza kulifanyia kazi suala la ujenzi wa kingo za mto Kanoni, ambao utaondoa kabisa changamoto ya mafuriko hapa Bukoba Mjini.”
Dkt. Samia amesisitiza kuwa Serikali imeweka kipaumbele katika kulinda maisha na mali za wananchi, na kwamba mradi huo ni sehemu ya mpango mpana wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mbali na hilo, Dkt. Samia amegusia pia umuhimu wa kuboresha miundombinu ya barabara katika Jiji la Bukoba, akisema Serikali imeidhinisha ujenzi wa barabara zenye jumla ya kilomita 10 kwa kiwango cha lami, sambamba na ufungaji wa taa za barabarani 413 ili kuimarisha usalama wa usafiri na urembo wa mji.
