Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mji Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, ametoa rai kwa viongozi wa kata na mitaa kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, ili wananchi waweze kunufaika moja kwa moja na huduma bora za kijamii.
Ameeleza viongozi wa ngazi hizo wanapaswa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo, kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na kuhimiza uwajibikaji miongoni mwa watendaji waliopo chini yao.

Aidha, Dkt. Shemwelekwa aliwataka wananchi wa Manispaa hiyo kutunza miundombinu na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, akisisitiza kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika kuboresha huduma za jamii, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha inahifadhiwa.
“Haipendezi kuona serikali inatoa fedha nyingi kutekeleza miradi ya maendeleo lakini wananchi hawatunzi miundombinu hiyo,” alisema Dkt. Shemwelekwa.
“Kwa mfano, Manispaa ya Kibaha imetoa shilingi milioni 420 kwa ajili ya kutengeneza barabara, lakini changamoto kubwa imekuwa wananchi kutokutunza barabara hizo mara baada ya kufunguliwa.”

Aliongeza kuwa miradi ya serikali ni matokeo ya kodi za wananchi, hivyo kuitunza ni sehemu ya uwajibikaji wa jamii katika kuendeleza maendeleo.
“Kama leo tumefungua barabara, basi mwaka ujao tuweke kifusi na kuendelea kuboresha zaidi ili tuendelee kupiga hatua za kimaendeleo,” alisisitiza Shemwelekwa.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kata za Picha ya Ndege na Mbwawa, akiwa ameambatana na Wakuu wa Divisheni na Vitengo mbalimbali, ambapo alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

Katika Kata ya Picha ya Ndege, Dkt. Shemwelekwa alitembelea miradi ya uchongaji barabara yenye thamani ya shilingi milioni 30 (mapato ya ndani), ujenzi wa vituo vya kibiashara kwa mbonde (milioni 562.5), na ukamilishaji wa chumba kimoja cha darasa katika Shule ya Msingi Lulanzi (milioni 8).
Alikagua pia maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Hospitali ya Wilaya (thamani ya milioni 706.7 kupitia mapato ya ndani na Serikali Kuu), ununuzi wa vifaa tiba (milioni 300 Serikali Kuu), ujenzi wa Ofisi ya Kata ya Picha ya Ndege (milioni 24.5) na darasa moja katika Shule ya Msingi Mkuza (milioni 20).
Kwa ujumla, alikagua miradi minane (8) yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.6, ikiwemo miradi inayotekelezwa kupitia mapato ya ndani pamoja na michango kutoka Serikali Kuu.

Katika ziara hiyo, Dkt. Shemwelekwa pia alifanya mkutano wa hadhara kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa Kata ya Picha ya Ndege, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na jamii katika kusukuma mbele maendeleo.
Wananchi wa kata hizo walimpongeza Mkurugenzi huyo kwa kufuatilia miradi kwa ukaribu na kwa kujitokeza kusikiliza changamoto zao, wakisema kuwa anaonesha uwajibikaji, kasi na ufuatiliaji wa karibu katika kusimamia maendeleo ya Mji Kibaha.




