Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameongoza majadiliano muhimu yaliyoandaliwa na UN Women kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, yaliyolenga kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazowakabili wanawake na wasichana duniani.

Majadiliano haya yamefanyika leo, tarehe 24 Julai 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Mjadala umejikita katika kuainisha mikakati bora ya kutekeleza ahadi zilizowekwa katika Ajenda ya 2030, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, pamoja na Azimio la Beijing.

Aidha, washiriki wamebainisha kuwa changamoto kama ukosefu wa elimu na mifumo dhaifu ya afya zinaweza kutatuliwa iwapo jamii zitajitahidi kulinda mafanikio yaliyopatikana, kwa kuimarisha mifumo ya kisheria, kisiasa na kifedha kwa ajili ya kuendeleza usawa wa kijinsia.

Katika mchango wake, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesisitiza umuhimu wa kuweka usawa wa kijinsia na utekelezaji wa Ajenda ya 2030 kuwa vipaumbele vya kimataifa, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuungana katika kukabiliana na vikwazo vinavyokwamisha juhudi za Umoja wa Mataifa katika kuwawezesha wanawake na wasichana. Amesisitiza kuwa “wakati wa kuchukua hatua ni sasa”, hasa wakati ambapo dunia inakabiliwa na changamoto nyingi zinazotishia maendeleo ya kijinsia.