Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia Dodoma
Dr. Tulia Ackson Mwansasu, aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametangaza kujiondoa rasmi kwenye kinyang’anyiro cha Uspika wa Bunge leo, hatua iliyotangazwa kupitia taarifa yake binafsi kwa umma.
Uamuzi huo umekuja ghafla na bila maelezo ya kina, hali iliyozua mjadala mpana miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wanasiasa na wananchi wanaofuatilia mwenendo wa Bunge la Tanzania.
Dr. Tulia ambaye amehudumu kama Spika wa Bunge tangu Februari 2022, anajulikana kwa umahiri wake katika masuala ya sheria, uongozi na nidhamu ya Bunge.
Ikumbukwe Kabla ya kuingia rasmi katika siasa, alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Shule ya Sheria, na baadaye akajipatia Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini.
Safari yake ya uongozi ilianza mwaka 2015 alipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza na kisha kuteuliwa kuwa Naibu Spika kabla ya kuchukua nafasi ya juu ya Uspika.
Mbali na nafasi hiyo, Dr. Tulia amejizolea heshima kimataifa baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (Inter-Parliamentary Union – IPU) mnamo Oktoba 2023, akiwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kushika wadhifa huo.
Uwepo wake katika jukwaa hilo la kimataifa umechukuliwa kama hatua kubwa kwa Tanzania katika kukuza ushiriki wa wanawake kwenye uongozi wa kisiasa.
Hata hivyo kujiondoa kwake kwenye mbio za Uspika kumefasiriwa na wachambuzi kama ishara ya mabadiliko ya kimkakati ndani ya mfumo wa uongozi wa Bunge.
Wakati bado haijajulikana hatma na kiini cha kujiondoa kwake kwenye kinyang’anyiro hicho wengi wanaamini kuwa uzoefu na umahiri wake katika masuala ya sheria na uongozi vitabaki kuwa nguzo muhimu katika mchango wake kwa Taifa.


