Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepongezwa kwa kuendelea kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija na faida kwa wakulima na wananchi kwa ujumla.

Pongezi hizo zimetolewa na, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua warsha kuhusu kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Kilimo  leo tarehe 16 Julai, 2025 katika Ukumbi wa Mbaraka Mshee – Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, mkoani Morogoro.

“Mpango mwingine ni  Mpango wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Mpango kazi wa Mwaka wa Wizara na Taasisi (M&E Plan), Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (M&E Strategy) na Moduli ya kupima utendaji wa Wizara na Taasisi husika (M&E Performance Model). Aidha, ni muhimu kupima hali ya utayari wa kila Wizara na Taasisi zake,” alieleza .

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu imekasimiwa jukumu la kuratibu, kufuatilia, kutathmini na kupima utendaji wa serikali nchini hivyo ofisi imeendelea kuratibu shughuli hizo kwa kuandaa na kuwasilisha nyaraka muhimu zitakazowezesha ubora na ufanisi wa kazi za ufuatiliaji na tathmini. 

“Ni muhimu kuvisimamia vitengo vyenu kutekeleza majukumu yao kwa kufuata miongozo ili kazi zetu ziwe na ubora unaotakiwa. Aidha, ni matarajio yangu kuwa nyaraka hizo zitawaongoza kuandaa nyaraka elekezi na tendaji kwa kuzingatia muktadha wa Wizara yenu ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yenu,” alibainisha.

Aidha, Dkt. Yonazi aliwasihi washiriki wa warsha hiyo  kujadili masuala yote ikiwemo changamoto zinazoweza kusababisha kuwa na utekelezaji usioridhisha katika Wizara mbalimbali na Taasisi zake ikiwemo Wizara ya Kilimo pamoja na kupendekeza namna bora ya kuondokana na changamoto hizo.