Na Mwandishi Wetu JamhuriaMedia,Katavi

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amezitaka Bodi za Wadhamini zinazosimamia taasisi zisizo za kiserikali, taasisi za kidini, michezo na taasisi nyingine zinazotoa huduma kwa jamii kujiepusha na vitendo vya ubadhirifu wa mali na migogoro isiyo ya lazima, na badala yake kusimamia mali za taasisi wanazoziongoza kwa uadilifu, uwajibikaji na kwa kuzingatia sheria.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo ulioandaliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa ajili ya kuwajengea Uwezo Wajumbe wa Bodi za Wadhamini na watendaji wa Serikali kutoka mikoa ya Katavi, Kigoma, Tabora, Mbeya, Rukwa na Songwe, uliofanyika katika Hoteli ya Home Alone mkoani Katavi.

Dkt. Homera amesisitiza kuwa wadhamini wana wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Bodi za Wadhamini Sura ya 318, akionya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale watakaokiuka sheria, kujimilikisha mali, kufanya ubadhirifu au kukaa madarakani kinyume na katiba za taasisi zao.

“Bado ipo changamoto ya baadhi ya bodi za wadhamini kutotimiza majukumu yao kikamilifu kwa kutumia mali za taasisi kwa maslahi binafsi, kufanya ubadhirifu wa mali na fedha, kujimilikisha mali kinyume cha utaratibu, bodi za Wadhamini kukaa madarakani zaidi ya muda ulioainishwa katika Katiba hivyo kusababisha migogoro na uvunjifu wa amani;” amesema Dkt. Homera.

Hata hivyo, amempongeza Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Frank Kanyusi kwa hatua mbalimbali anazozichukua kwa lengo la kutatua na kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika Bodi za Wadhamini.

“Nafahamu kwamba ipo migogoro kadhaa ambayo ni ya muda mrefu na imeshafikishwa katika wizara yangu na ngazi nyingine za kitaifa,” Lakini napenda.

Wadhamini wote mfahamu kwamba hatua stahiki za kisheria na kiutawala zitachukuliwa kwa wale wote wanaokiuka misingi ya Sheria katika utekelezaji wa majukumu yao na kusababisha migogoro hii kuendelea;” amesema.

Amezitaka bodi hizo za wadhamini kuwasilisha taarifa za utendaji wao RITA kupitia mfumo wa kidijitali na kufanyia matrekebisho katiba zao ili kuendana na wakati na matarajio ya taasisi zao.

Ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na taasisi zake imedhamiria kuhakikisha kila taasisi inasimamiwa na Bodi ya Wadhamini yenye uadilifu, ujuzi na uwezo wa kuhakikisha mali na rasilimali za taasisi zinafanya kazi kwa manufaa ya wanachama.

Aidha, ametoa maelekezo kwa RITA kuharakisha marekebisho ya sheria husika, kuendelea kuboresha mfumo wa kidijitali wa eRITA, kuanzisha huduma za Mobile Clinics nchi nzima ili kusogeza huduma karibu na wadau, pamoja na kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa umma na wadhamini kuhusu majukumu yao ya kisheria.

Miongoni mwa maagizo aliyoyatoa kwa RITA, Dkt. Homera ameitaka taasisi hiyo Kufanya Tathmini ya mikutano ya wadau inayoifanya, ili kubaini changamoto zinazojitokeza na kuzifanyia kazi katika mikutano mingine.

Pia ameilekeza RITA kushirikiana na wadau wengine ili iongeze kasi ya utoaji elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bodi za wadhamini kufuata misingi ya sheria na kanuni na vilevile jamii kujua umuhimu wao katika usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya bodi za wadhamini.

Kwa upande wake, Kanyusi Frank, amesema hadi kufikia Februari 10, 2026, jumla ya Bodi za Wadhamini 5,211 zimesajiliwa nchini. Kati ya hizo, 2,876 ni za taasisi za kijamii, 2,161 za kidini, 19 za vyama vya siasa, 24 za michezo na 150 za kifamilia.

Aidha, Kabidhi Wasii Mkuu ameweka wazi kwamba Wadhamini wamepewa mamlaka na kuaminiwa kusimamia mali za Taasisi kwa faida ya wanachama au wanufaika kulingana na madhumuni ya kuanzishwa taasisi husika kama yalivyoainishwa katika katiba.

“Hii inamaanisha ukiwa mdhamini unatakiwa kuhakikisha mali za wanachama zinalindwa na kutumika kwa matumizi sahihi yalioainishwa katika Katiba ya taasisi husika,” amesema Bw. Kanyusi.