Jumuiya ya wanadiplomasia nchini imetakiwa kufikisha taarifa katika Serikali za nchi zao kuwa Dodoma ipo tayari na kwamba Serikali hizo zinatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi na makazi ya balozi kwenye viwanja vilivyotolewa bure kwenye mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) kwenye Mkutano maalum wa Jumuiya ya Wanadiplomasia nchini uliondaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kufanyika jijini Dodoma Mei 27, 2025.
Waziri Kombo aliwaeleza Mabalozi hao kuwa siri kubwa ya mafanikio yoyote duniani ni kuwa na imani na jambo unalolidhamiria kulitekeleza. Serikali ya Tanzania tangu ilipofanya uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya nchi jijini Dodoma mwaka 1973 ilikuwa na imani na uamuzi huo na leo imani hiyo inatekelezwa kivitendo kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika maeneo ya miundombinu na huduma za kijamii ili kuuweka mji wa Dodoma katika mazingira mazuri ya kuishi, kwa watu wa aina yote, wakiwemo Mabalozi.
Balozi Kombo alisema kutokana na ujenzi wa mji wa Dodoma, fursa nyingi za uwekezaji zimeibuliwa, hivyo ametoa wito kwa Mabalozi kuwaleta wawekezaji jijini Dodoma kuchangamkia fursa hizo. Ametoa wito pia kwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoa taarifa ya kila hatua ya ujenzi wa mji huo kwa wadau kwa lengo la kuwahamasisha kufanya uamuzi sahihi kuhusu Dodoma. Alisema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kupeana taarifa kuhusu maendeleo ya mkoa wa Dodoma na kupendekeza uwe unafanyika kila mwaka.
Mwenyeji wa Mkutano huo uliobeba kaulimbiu “Dodoma Ipo Tayari: Ipeleke Dodoma Duniani na Ilete Dunia Dodoma”, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule alitumia jukwaa hilo kueleza hatua mbalimbali zilizofikiwa katika ujenzi wa mji huo, hususan katika maeneo ya miundombinu ya huduma za afya, elimu, maji, umeme, usalama, usafiri na burudani. Alusema huduma hizo zinapatikana kwa ubora wa kimataifa, hivyo jumuiya ya wanadiplomasia isihofie chochote inakaribishwa Dodoma na Dodoma ipo tayari kwa ajili yao.
Mhe. Mkuu wa Mkoa pia alibainisha fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana jijini Dodoma katika sekta za kilimo, utalii, logistics, viwanda & ujenzi na madini na kuwakaribisha wawekezaji kuchangamkia fursa hizo.
Alisema Serikali ipo katika mchakato wa kujenga Hombolo Thermatic Satelite City na kubainisha kuwa hiyo ni fursa kubwa na adhimu kwa wawekezaji kushirikiana na Serikali kufanikisha ujenzi wa mji huo.
Naye, Mwakilishi wa Kiongozi wa Mabalozi ambaye alikuwa Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Isaac Njenga alisema kuwa yeye na Mabalozi wenzake wameshuhudia hatua kubwa iliyopigwa katika ujenzi wa mji wa Dodoma hasa baada ya kutembelea na kujionea mji wa Serikali uliopo eneo la Mtumba, Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato. Amesema kwa niaba ya Mabalozi wenzake wameridhika na hatua iliyofikiwa na wameahidi kuzishawishi Serikali za nchi zao kutenga fedha za kuanza ujenzi wa ofisi na makazi ya balozi jijini Dodoma.
Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wapo jijini Dodoma kushiriki uwasilishaji wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 tarehe 28 Mei 2025.



