Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amekagua utekelezaji wa Mradi wa kusimika Kamera za usalama (CCTV) katika jiji la Dodoma, mradi unaogharimu shilingi milioni 473 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mradi huo unahusisha ufungaji wa nguzo 50 zitakazobeba kamera 106 zenye uwezo wa kisasa wa kusoma namba za magari, kutambua sura za watu, kuhesabu vyombo vya usafiri na watu, pamoja na kubaini makosa ya barabarani ikiwemo magari yaliyopaki maeneo yasiyoruhusiwa.

Akizungumza Mara alipotembelea Mradi huo Senyamule amesema uwepo wa kamera hizo utaleta heshima na usalama kwa jiji la Dodoma, kuongeza ufanisi wa vyombo vya dola na kuwapa wananchi pamoja na wawekezaji uhakika wa kuishi na kufanya biashara katika mazingira salama.
Aidha, amehamasisha Taasisi na Mashirika mbalimbali kuiga mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kuwekeza kwenye mifumo ya ulinzi wa kisasa huku akiahidi kuendelea kusimamia amani na utulivu ya mkoa hususan katika kipindi cha uchaguzi, akisisitiza kila mwananchi kutimiza haki kwa kufuata sheria za nchi.
Kwa uoande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri, amesema mradi huo ni chachu ya mageuzi makubwa katika usimamizi wa usalama wa barabarani na maeneo ya mikusanyiko mikubwa, kwa kuwa kamera zitaweza kurekodi na kutoa taarifa za moja kwa moja kwa vyombo vya dola.
Ametaja maeneo ambayo Kamera hizo zimekusudiwa kufungwa kuwa ni katika njia kuu nne zinazoingia na kutoka jijini, maeneo ya katikati ya jiji, Machinga Complex pamoja na Nala, ili kuimarisha ulinzi wa raia, mali zao na miundombinu ya umma.

Pia amesema Kamera zitasaidia kudhibiti vitendo vya jinai na uharibifu wa miundombinu, hasa kwa kuzingatia Dodoma kama makao makuu ya nchi inabaki salama kwa uwekezaji na kuongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo ni chachu inayotokana na ziara ya mafunzo maalum nchini China katika mji wa Guanzhou ili kuongeza umahiri wa uendeshaji wa mfumo huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Wisjane Smart System, Wisley Ussiri, ambao ndiyo watekelezaji wa Mradi,amesema kamera zitakazowekwa ni za aina tatu ambazo ni zinazosoma namba za magari, zinazofuatilia mienendo ya watu na zile zinazoweza kunasa matukio kwa umbali wa viwanja 45 vya mpira sawa na kilomita 4.5.
Ussiri amebainisha kuwa mfumo huu utasaidia askari polisi kwa kiwango kikubwa katika kudhibiti uhalifu, hasa ikizingatiwa changamoto ya idadi ndogo ya askari wa iliyopo kwani kamera zitakuwa zikifanya kazi usiku na mchana na kuhifadhi kumbukumbu kwa muda mrefu.


